Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela Reuters |
Na Flora Martin Mwano
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson Mandela amelazwa hospitalini kwa
mara nyingine tena akiendelea kusumbuliwa na maradhi ya mapafu.
Taarifa iliyotolewa katika tovuti ya Ofisi ya Rais nchini humo
imebainisha kuwa kiongozi huyo amefikishwa hospitalini mjini Pretoria
baada ya hali ya afya yake kudhoofika tena.
Msemaji wa Rais Jacob Zuma, Mac Maharaj amesema Mzee Mandela
anashughulikiwa na Madaktari Bingwa ambao wanafanya kila jitihada
kuhakikisha kiongozi huyo mzalendo anapata nafuu.
Mapema mwezi April mwaka huu Mandela alikaa hospitalini kwa takribani
siku kumi akikabiliwa na maradhi yatokanayo na kuathirika kwa mapafu
yake hali inayotajwa kuchangia kuzorotesha afya yake kwa muda mrefu
sasa.
Mandela ambaye sasa ana umri wa miaka 94 amekuwa akisumbuliwa na maradhi
kwenye miaka ya hivi karibuni ambapo mara kadhaa amefikishwa hospitali
kwa matibabu ya maradhi kama hayo ambayo madaktari wanasema yanatokana
na umri wake kuwa mkubwa. Via kiswahili.rfi.fr
Comments