Na Bosire Boniface, Garissa
Chini ya agizo la serikali mpya, huduma za uzazi kwa sasa ni bure katika
hospitali za umma, vituo vya afya na kwenye kliniki nchini Kenya,
lakini baadhi ya vituo vya kutoa huduma za afya bado havifuati agizo
hili la msamaha wa ada zinazohusiana na uzazi.
Mwanamke akiwa na mtoto akitembea karibu na tangazo kuonyesha Hospitali ya Mathari huko Nairobi. [Simon Maina/AFP]
"Serikali yangu imefanya mipangilio ya bajeti inayotosha kuwezesha akina
mama wote wajawazito kupata huduma za uzazi bure katika vituo vya afya
vya umma, kuanzia tarehe 1 Juni, 2013," Rais Uhuru Kenyatta alisema
katika kulihutubia taifa Siku ya Madaraka, kufuatia ahadi ya kampeni ya
Muungano wa Jubilee aliahidi kutekeleza wakati wa siku 100 za mwanzo
madarakani.
Fedha zilizowekwa katika bajeti ya mwaka 2013-2014 zinawapa Wakenya wote
fursa nzuri ya kupata huduma za msingi za afya kwenye vituo na zahanati
zinazoendeshwa na serikali, rais alisema.
Kenyatta pia alifuta ada ya shilingi 10 (senti 12 ) na shilingi 20
(senti 23), ambayo zahanati na vituo vya afya vimekuwa vikitoza
wagonjwa.
Hata hivyo, baadhi ya vituo vya afya vimeendelea kutoza akina mama wanaokwenda kujifungua watoto wao.
"Wakati agizo la rais linatolewa, kwa kawaida tunapaswa kusubiri waraka
kutoka wizarani ukitoa maelekezo," Mrakibu wa Hospitali ya Mbagathi huko
Nairobi Daktari Andrew Sule aliiambia Sabahi. "Wakina mama wanaokuja
kujifungua watapaswa kulipa hadi tutakapopokea mawasiliano rasmi."
Comments