Dodoma. Zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya Bajeti Kuu ya Serikali
kusomwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi
Magharibi (CCM), Andrew Chenge amesema Serikali imeelemewa na mzigo wa
madeni.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa anatarajia kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 keshokutwa.
Chenge alisema hayo juzi Mjini Dodoma baada wa mkutano wa majadiliano ya
namna bora ya utendaji kazi baina ya Kamati ya Bunge ya Bajeti na
kamati za Miundombinu, Ulinzi na Usalama, Mambo ya Nje, Hesabu za
Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).
Alisema Serikali imeelemewa na madeni huku kila wizara ikitaka
kukamilishiwa mafungu yake ya fedha jambo ambalo linashindikana kwa kuwa
hazipo.
Kwa mujibu wa hotuba ya Kambi ya Upinzani ya Wizara ya Fedha, mpaka sasa
deni la taifa limefikia Sh21.028 trilioni bila dhamana ya Serikali kwa
mashirika ya umma na binafsi hadi kufikia Desemba 2012 na kati ya fedha
hizo, asilimia 75.97 ni deni la nje.
Hata hivyo, katika majibu ya Serikali, Waziri Mgimwa alisema Serikali
imeanza kulipa na kuanzia Julai 2012 hadi Aprili 2013, malipo ya madeni
yamefikia Sh1,666.77 bilioni na kati ya hizo, deni la nje lililolipwa ni
Sh213.57 bilioni.
Comments