Mbowe asema walilenga kumuua na Lema
Nassari ashambuliwa, ajeruhiwa, alazwa
Polisi waendelea kuunda timu za makachero
Matukio ya ugaidi yanazidi kutikisa nchi, huku hofu kubwa ikitanda
miongoni mwa jamii kwa kuwa juhudi za kuwasaka wahusika hazionyeshi
kuzaa matunda na wala umma hauelezwi taarifa zozote juu ya uchunguzi
wake.
Ugaidi uliofanywa dhidi ya mkutano wa kufunga kampeni za udiwani wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jijini Arusha juzi ni
limetokea takribani siku 40 tu baada tukio jingine lilinalofanana nalo
kwa kila kitu, kutokea kwenye hafla ya uzinduzi wa Parokia ya Olasiti ya
kanisa Katoliki Mei 5, mwaka huu jijini Arusha pia.
Katika shambulizi la kanisani, bomu lilirushwa kwenye mkusanyiko mkubwa
wa waumini nia ikiwa ni kuangamiza watu wengi, hata hivyo walikufa watu
watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60.
Ingawa hadi sasa polisi hawajatoa taarifa kwa umma juu ya aina ya bomu
lililolotumika Olasit, mlipuko wa juzi kwenye mkutano wa Chadema,
unafanana kwa kila kitu na ule wa Mei 5, mwaka huu.
Wakati Olsasit walengwa wakuu alikuwa Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa
Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla na
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu, juzi
walengwa walitaka kuwaua pamoja na watu wengine Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Mfululizo wa matukio haya ya ugaidi mbali ya kuasababisha kuahirishwa
kwa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne jijini Arusha, pia
umekifanya Chadema kusitisha mahudhurio ya wabunge wake wote katika
vikao vya Bunge kuanzia leo na kwamba wanatakiwa kwenda Arusha kwa ajili
ya shughuli za maziko ya watu wawili waliouawa katika mlipuko wa bomu
uliotokea juzi jijini Arusha.
Comments