Rais John Magufuli juzi aliwazungumzia makada walioihama CCM wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita, alipoeleza kuwa kuondoka kwao pengine kulimsaidia kupata ushindi.
Bila kutaja majina ya waliokihama chama, Magufuli alisema ni vyema wana CCM wakasahau tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo na kuganga yajayo.
Rais alisema hayo kwenye mkutano na viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya zote nchini, uliofanyika juzi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Alisema kuna mengi yalitokea wakati wa uchaguzi huo na yalikidhoofisha chama na hivyo kuna haja ya kuyasahau yaliyopita na kuangalia mbele katika kukijenga chama.
“Lakini inawezekana wale walioamua kwenda kule walisaidia mimi kushinda,”alisema bila ya kufafanua.
Baadhi ya wana CCM waliokihama chama hicho wakati wa uchaguzi huo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa kuanzia ndani ya chama hicho ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowasa aliyehamia Chadema, Frederick Sumaye, ambaye kwanza alitangaza kujiunga na upinzani bila ya kutaja chama na mapema mwaka huu kukabidhiwa kadi ya Chadema.
Mwingine ni aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, Balozi Juma Mwapachu, mawaziri, wabunge na madiwani, wengi wakijiunga na Chadema, ambayo ilimsimamisha Lowassa kuwa mgombea wake wa urais akiungwa mkono na vyama vya NLD, NCCR-Mageuzi na CUF vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Lowassa alionekana kuwa kinara kwenye harakati za urais ndani ya CCM, akichuana vikali na Bernard Membe, lakini jina lake halikufikishwa kwenye Kamati Kuu, ambayo ilitangaza majina matano, akiwamo Magufuli, yaliyopelekwa Halmashauri Kuu ya chama hicho.
Kitendo hicho kilifanya wajumbe wa Halmashauri Kuu kumpinga waziwazi mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete na baada ya juhudi za wazee wa chama hicho, hali ilitulia na Magufuli akaongoza kwa kura nyingi. Baadaye Lowassa alitangaza kuhamia Chadema na kufuatiwa na wanachama kadhaa.
Alipotangazwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu, Magufuli alisema wakati akihutubia wanaCCM kwenye ofisi ndogo ya chama hicho Lumumba jijini, alisema uchaguzi huo ulikumbwa na hujuma zilizofanywa na wanafiki waliojificha ndani ya chama hicho.
Alisema ni vema wanafiki hao wakajisalimisha kwa kutubu kwa kuwa wamekigharimu chama hicho na kusababisha kiwe kwenye wakati mgumu.
Dk Magufuli alisema anaona ni bora kuishi na mchawi kuliko mnafiki, na kumuomba Kikwete asiwahurumie wanaokihujumu chama.
CCM walikidhoofisha chama
Juzi, akizungumza kwenye mkutano huo na viongozi wa CCM ambao katika hali isiyokuwa ya kawaida hawakuvaa sare zao za chama, Magufuli alisema waliokidhoofisha chama ni wana CCM wenyewe na ndiyo maana wapinzani walitumia udhaifu huo kukisaliti.
“Tulithamini fedha kuliko chochote. Wala hatukuuliza hizi fedha zimetoka wapi. Tuliowapa miradi, walituchezea, tumejikaanga CCM kwa mafuta yetu wenyewe. Kama tulifanya makosa, tusifanye tena,” alisema.
Aliwataka viongozi hao wa CCM kuanza kuzungukia maeneo yao ili kuwashukuru wananchi kwa ushindi na kukiimarisha chama.
“Kwa kifupi, nyinyi ndiyo Serikali. Kiongozi yeyote mnayemuona hatekelezi ilani yake, huyo hafai kwenye safari hii. Mimi niwaahidi hatutasita kuchukua hatua kwa wale mtakaoona hawafai,” alisema.
Awali Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana alisema Kamati Kuu ya CCM imepokea ripoti ya uchaguzi huo wa Oktoba 25 kutoka mikoa yote na wiki ijayo itafanyika tathmini ya maandalizi, mchakato wa kuwapata wagombea, matokeo, upigaji kura na utangazaji wa matokeo.
Azungumzia Watumishi Hewa CCM
Kadhalika, Magufuli alimtaka Kinana kuanza kuchukua hatua za kuondoa wafanyakazi hewa ndani ya chama hicho.
“Na mimi nina uhakika katibu mkuu hata kwenye chama wapo wafanyakazi hewa kwa sababu watu ni wale wale, ni Watanzania wale wale. Kwa hiyo na wewe uanze kuchukua hatua dhidi ya wafanyakazi hewa walioko kwenye chama,” alisema.
Alisema Serikali inatumia zaidi ya Sh583 bilioni kulipa mishahara, lakini mpaka sasa kuna wafanyakazi 7,700 hewa wakati uchambuzi bado ukiendelea.Inatoka Udaku Specially
Comments