Katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon Ijumaa (22.04.2016) amemuwekea
mbinyo zaidi kiongozi wa waasi nchini Sudan kusini Riek Machar kurejea
mjini Juba "bila kuchelewa" na kuanza kazi katika serikali ya mpito.
Machar
alitarajiwa kurejea katika mji mkuu siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa
makubaliano ya kisiasa yenye lengo la kumaliza vita vya miaka miwili,
lakini tofauti kuhusiana na mipango ya kiusalama mjini Juba
inachelewesha kurejea kwake.
Ban
amesema serikali ya rais Salva Kiir imekubali pendekezo la muafaka
kuhusiana na matayarisho ya kurejea kwa Machar na kusema hatua hii
inapaswa kusaidia kuundwa kwa haraka kwa serikali mpya ya umoja wa
kitaifa.
"Kuendelea
na hali ya ushirikiano itakuwa muhimu wakati viongozi wa nchi hiyo
wakianza mchakato wa kubadilisha miaka ya uharibifu uliosababishwa na
mzozo huo kwa watu wa Sudan kusini," amesema katika taarifa.
Mateso ya watu wa Sudan kusini
Ban
amemtaka Machar kusafiri kwenda Juba " bila masharti zaidi" hali ambayo
inaweza kuchafua mchakato wa amani na kuendeleza hali ya mateso
yanayowakuta watu wa Sudan kusini."(P.T)
Chini ya
makubaliano ya amani, Machar alitakiwa kurejea tena katrika wadhifa wake
wa makamu wa rais katika serikali mpya itakayodumu kwa muda wa miezi 30
na kuielekeza nchi hiyo katika uchaguzi mkuu.
Kikwazo
cha hivi sasa kinahusiana na idadi ya bunduki na vifaa vya kufyatulia
maguruneti ambavyo vikosi vya waasi vinavyomlinda Machar vitaruhusiwa
kuwa navyo.
Vita vya
Sudan kusini vilianza Desemba mwaka 2013, wakati Kiir alipomshutumu
Machar kwa kula njama za kumpindua. Mzozo huo umeweka wazi mpasuko wa
tofauti za kikabila na umekuwa ukionesha ukiukaji mkubwa wa haki za
binadamu, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa makundi, uchomaji moto vijiji na
hata ulaji nyama za watu.
Ombi la Marekani
Kwa ombi
la Marekani, baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana siku ya
Jumatatu na kuelezea "wasi wasi wake mkubwa " kwa kushindfwa kurejea
Machar mjini Juba.
Jumuiya
zenye nguvu duniani, ikiwa ni pamoja na Umoja Umoja wa Afrika, Umoja wa
Ulaya , China , Uingereza na Marekani , zimewapatia Machar na Kiir muda
wa mwisho hadi leo Jumamosi (23.04.2016) kutatua tofauti zao.
Mamia kwa
maelfu ya watu wameuwawa na zaidi ya watu wengine milioni mbili
wamelazimika kuyakimbia makaazi yao tangu vita hivyo vilipozuka Desemba
mwaka 2013.
Wasiwasi unatuwama katika hali ya kutoaminiana kuhusiana na silaha hali ambayo imechelewesha kurejea kwa Machar.
Kikosi
cha wanajeshi waasi wapatao 1,370 tayari kimewasili mjini Juba kama
sehemu ya makubaliano ya amani wakati majeshi ya serikali yanasema
yameondoa wanajeshi wake wote isipokuwa wanajeshi 3,420 , kwa mujibu wa
makubaliano. Wanajeshi wengine wote wanapaswa kubakia kiasi ya kilometa
25 nje ya mji mkuu.
Katika
moja kati ya kambi tatu za waasi mjini Juba, waasi wanatengana na kambi
ya majeshi ya serikali kiasi ya mwendo wa miguu wa dakika tano na
wanaweza kuonana na karibu iwapo kutatokea rabsha zozote.
Chanzo:DW
Comments