Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Ephraim Mgawe, pamoja na aliyekuwa Naibu wake, Hamad Koshuma, wanaokabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka wamepatikana na kesi ya kujibu.
Mgawe na mwenzake wanakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kutoa zabuni kwa kampuni ya China, China Communication Construction Company Limited, kwa ajili ya ujenzi wa maghati katika Bandari ya Dar es Salaam.
Leo mahakama katika uamuzi wake baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka iliwaona kuwa wana kesi ya kujibu kwa mashtaka yanayaowakabili na hivyo kuwataka kupanda kizimbani kujitetea, Mei 16 mwaka huu.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkazi Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo alisema kwamba ameridhika kuwa upande wa mashtaka umeweza kujenga kesi dhidi ya washtakiwa hao na kuwa wana kesi ya kujibu.
“Baada ya kupitia ushahidi wa uliowasilishwa na uapnde wa mashtaka pamoja na vielelezo nimeridhika kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu, hivyo wanatakiwa kutoa utetezi wao.”, alisema Hakimu Mkeha.
Baada uamuzi huo, Mgawe aliieleza Mahakama kuwa anatarajia kuita mashahidi tisa kumtetea mahakamani hapo, huku Koshuma akisema akisema kuwa yeye atajitetea mwenyewe na kwamba hatakuwa na shahidi mwingine.
Mgawe na Koshuma wanadaiwa kula njama na kutoa zabuni tata kwa kampuni hiyo ya Kichina kwa ajili ya kujenga maghati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa gharama ya Dola 600 milion, kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mkataba wa kibiashara na kampuni hiyo ya Kichina bila zabuni shindanishi kinyume cha sheria hiyo ya manunuzi ya umma.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka namna ambavyo zabuni hiyo ilivyotolewa kwa kampuni hiyo washtakiwa hao walikuwa na maksudi ya kujipatia manufaa kwa kampuni hiyo ya Kichina.
Upande wa mashtaka unaendelea kudai kuwa kitendo hicho cha washtakiwa walikiuka masharti ya kifungu cha 31 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma, namba 21 ya mwaka 2004.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwaita mahakamani jumla ya mashahidi watano kujenga kesi yao, akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa mamlaka hiyo, Kokutulage Kazaura.
Katika ushahidi wake Kazaura alidai kuwa mkataba baina ya kampuni hiyo na mamlaka hiyo December 5, 2011, na Mkurugenzi Mtendaji, Mgawe, ukishuhudiwa na naibu wake Koshuma.
Shahidi huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa walishindwa kufuata mchakato wa manunuzi kwa kuwa tayari TPA ilikuwa imeshaingia katika makubaliano na kampuni hiyo, na kwamba kwa hali hiyo hapakuwa na haja ya kutangaza zabuni.
Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kutoa uamuzi wa uhalali wa shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA,
Harry Msamire Kitilya, na wenzake wawili.
Mbali na Kitilya washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mshindi wa Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania), mwaka 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon.
Washtakiwa kupitia kwa mawakili wao walihoji uhalali wa shtaka hilo na kuiomba mahakama ilifute pamoja na mambo mengine wakida kuwa halijakidhi vigezo vya kisheria kuitwa shtaka la utakatishaji fedha.
Maombi yao hayo yalitarajiwa kutolewa uamuzi jana na Hakimu Mkazi Emilius Mchauru, anayesikiliza kesi hiyo, lakini uamuzi huo ulikwama na badala yake ulipigwa kalenda hadi April 27 mwaka huu.Inatoka Udaku Specially.
Comments