Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kiingilio cha
shilingi elfu mbili tu (2,000) ndio kitakachotumika katika mchezo wa
kesho Jumamosi kati ya Serengeti Boys (Tanzania) v The Pharaohs (Misri)
katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
TFF imeweka kiingilio cha shilingi elfu mbili tu (2000) uwanja mzima,
kutoa nafasi kwa wapenzi wa mpira wa miguu nchini kujitokeza kwa wingi
siku ya Jumamosi kuja kushuhudia mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa
kati ya timu za vijana za Tanzania vs Misri.
Serengeti Boys inashuka dimbani kucheza na The Pharaohs mchezo wa
kirafiki wa kimataifa wa kujipima nguvu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi
na kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika
kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi ya Shelisheli Juni – Julai
mwaka huu.
Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa utachezeshwa na waamuzi wa
kimataifa wenye beji za FIFA ambao ni Israel Mjuni, akisaidiwa na Soud
Lila, Frank Komba, mwamuzi wa akiba Jonesia Rukyaa, huku kamisaa wa
mchezo akiwa Isabella Kapera.
Upande wa kikosi cha timu ya Taifa ya Misri kimewasili nchini jana
mchana saa 7:30 mchana kwa shirika la ndege la Ethiopia, kikiwa na
msafara wa watu 33 wakiwemo wachezaji 25 na viongozi 8.
The Pharaohs wanatarajiwa kufanya mazoezi leo jioni saa 10 kamili
katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaa, baada ya kuwa wamefanya
mazoezi jana jioni katika uwanja wa Karume.
Wakiongea
na waandhishi wa habari, makocha wa timu zote mbili, Bakari Shime
(Serengeti Boys) na Yasser Muhamadain (The Pharaous) wameshukuru kwa
kupata mchezo huo wa kirafiki wa kiamataifa.
Kocha Shime ameishukuru TFF kwa kufanikisha mchezo huo wa kirafiki wa
kimataifa, baadaya kuwa kambini na kucheza michezo ya kirafiki na timu
za ndani, wao kama benchi la ufundi watautumia kama kipimo sahihi cha
mchezo wa kimataifa katika maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Shelisheli.
Naye Yasser wa The Pharaohs, ameshukuru kwa kupata nafasi ya kucheza
na Tanzania mchezo wa kirafiki, kwao ni mara ya kwanza kucheza mchezo wa
kirafiki nje ya ukanda wa Afrika Kaskazini, hivyo anaamini kesho
kutakua na mchezo mzuri wenye ushindani.
Comments