Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitangaza klabu ya
Mbao FC ya jijini Mwanza kupanda Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao
kutoka katika kundi C ya Ligi Daraja la Kwanza chini (StarTimes League).
TFF imeitangaza Mbao FC kfuatia maamuzi ya Kamati ya Nidhamu ya TFF
yaliyotolewa April, 2016 ya kuzishusha daraja timu nne kutoka kundi C
baada ya kukutwa na hatia ya upangaji matokeo.
Mbao FC imeshika nafasi ya kwanza kundi C kwa kuwa na pointi 12 baada
ya kufutwa kwa matokeo ya timu za Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Oljoro
na JKT Kanembwa zilizokumbwa na mkasa huo wa upangaji matokeo.
Timu ya Mbao FC inapanda ligi kuu (VPL) msimu ujao, sambamba na timu
za African Lyon ya jijini Dar es salaam pamoja na Ruvu Shooting ya mkoa
wa Pwani.
Wakati huo huo kikao cha Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF
kinatarajiwa kukaa Jumamosi ijayo April, 30 jijini Dar es salaam
kujadili rufaa mbalimbali ambazo zimekatwa na kutokana na maamuzi ya
kamati ya Nidhamu ya TFF.
Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya TFF itasikiliza rufaa za wafuatao waliokata rufaa
(i) Saleh Mang’ola,
(ii) Yusuph Kitumbo,
(iii) Amos Mwita,
(iv) Fateh Remtullah,
(v) Timu ya JKT Oljoro,
(vi) Timu ya Polisi Tabora.
Aidha Kamati ya Nidhamu ya TFF itakutana Jumapili Mei Mosi kupitia taarifa mbalimbali zilizowasiliswa katika kamati hiyo.
Comments