Shule ya Msingi Zanaki, iliyopo Manispaa ya Ilala, jijini Dar es
Salaam imeendelea kuongoza kwa ubora kitaaluma kwa mwaka wa pili
mfululizo baada kushika nafasi ya pili kwa darasa la saba kati ya shule
167 za msingi za serikali.
Pia Zanaki imeshika nafasi ya kwanza kwa ubora katika mitihani ya
darasa la pili ikiongozwa na Msimbazi Mchanganyiko kwa shule zote za
msingi katika manispaa hiyo.
Akitanganza ushindi wa Zanaki, Afisa Elimu Msingi wa Manispaa hiyo,
Elizabeth Thowa, alisema shule hiyo imeendelea kuwa kinara kitaaluma
baada ya wanafunzi wake kupata alama nyingi za A na B kwa masomo yote.
Alisema Zanaki imefanikiwa kushika nafasi ya 10 kwa ubora kitaaluma
kwa kushirikisha shule zote za serikali na binafsi kwa darasa la saba,
huku ikishika nafasi ya nne kwa ubora wa mitihani ya darasa la nne kwa
shule zote.
Thowa alikuwa akizungumza wakati wa kilele cha wiki ya Elimu na
Mazingira ya manispaa hiyo, iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja
ambako shule za msingi na sekondari za serikali na binafsi zilishiriki
na kutunukiwa zawadi ya vyeti, vikombe na vifaa vya usafi.
Mapema akizungumza katika hafla hiyo iliyotanguliwa na maandamano
yaliyopokelewa na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi,
Afisa Elimu (Sekondari), Violet Mlowosa, alisema maadhimisho hayo
hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujengea hamasa wanafunzi na walimu
kufanya bidii kitaaluma na kutunza mazingira.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Zanaki, Salim Mgamba, alisema shule
yake itaendelea ‘kutesa’ kitaaluma kwa sababu wazazi na walezi
wanasaidia kila kinachohitajika, hivyo kuwarahisishia walimu na viongozi
wa elimu manispaa hiyo kutimiza majukumu yake.
Chanzo: NIPASHE
Comments