Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi
ameitakia kila la kheri timu ya Young Africans katika mchezo wake wa
jumamosi wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CC) dhidi ya timu ya
Etoile du Sahel kutoka Tunisia, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika salamu zake kwa klabu ya Young Africans, Rais Malinzi
amewaambia wanapaswa kupambana na kuhakikisha wanapata ushindi katika
mchezo huo wa jumamosi, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga
mbele katika mchezo wa marudiano kwani ndio pekee kwa sasa
wanaoipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.
Young Africans imeingia katika hatua ya 16 bora Kombe l Shirikisho
barani Afrika,baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali
kwa jumla ya mabao (3-2), kisha kuwaondoa FC Platinum ya Zimbabwe katika
hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao (5-2).
Endapo timu ya Young Africans itafanikiwa kuwaondoa Etoile du Sahel
itasuburia kucheza mechi ya mtoano (Play-off) dhidi ya timu mojawapo
zitakaotolewa katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CL).
Wakati huo huo wapinzani wa Young Africans timu ya Etoile du Sahel
wanatarajiwa kuwasili saa 9 usiku kuamkia ijumaa kwa usafiri wa Ndege
ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair bj 4870 wakiwa na msafara wa watu
56.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tunisia (FTF),
Bw. Krifa Jalel ndiye mkuu wa msafara huo akiwa na Rais wa klabu ya
Etoile du Sahel (ESS) Bw.Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la
ufundi lenye watu 13, waandishi wa habari 12 na wanachama 10
Timu ya Etoile du Sahel itafikia katika hoteli ya Ledger Plaza zamani
Bahari Beach eneo la Kunduchi, na kesho jioni ijumaa wanatarajiwa
kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Waamuzi wa mchezo huo ni Samwel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio
de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide wote kutoka nchini Msumbuji na
wanatarajiwa kuwasili leo mchana, huku kamisaa wa mchezo huo Salah Ahmed
Mohamed kutokea nchini Sudan akitarajiwa kuwasili leo jioni na wote
watafikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.
Comments