Baada ya Kenya kuyafungia mashirika ya Kisomali kuendelea na shughuli
zao nchini humo mashirika ya misaada ya kibinadamu yameitaka Kenya
kuruhusu mashirika ya kusafirisha fedha ya Kisomali kuanza tena shughuli
zao ili kuwanusuru wakazi waishio Somalia.
Taarifa iliyotolewa na mashirika kama Oxfam, CARE, Mercy Corps, Adeso
na World Vision Somalia imesema kuwa familia za Kisomali zimepoteza
njia pekee rasmi, ya wazi na yenye nidhamu inayotumiwa kutuma na kupokea
fedha na kwamba mashirika yanayofanya kazi nchini Somalia pia
yanakabiliwa na hatari ya kukosa njia pekee ya kusafirisha fedha kwa
ajili ya kuendeshea shughuli zao za kibinadamu na operesheni za
maendeleo nchini Somalia.
Jumatano iliyopita serikali ya Kenya ilisimamisha vibali vya
mashirika 13 ya kusafirisha fedha ya Kisomali yaliyoko mjini Nairobi
katika juhudi za kuzuia fedha zisifikie kwa kundi la kigaidi la al
Shabab.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kundi hilo kuua watu wasiopungua 148
katika shambulizi lililolenga mabweni ya Chuo Kikuu cha Garissa huko
mashariki mwa Kenya.
Comments