Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, ametunukiwa
tuzo ya kutambua harakati zake za kutetea haki za binadamu katika
mazingira hatarishi nchini, likiwamo sakata la uchotwaji wa mabilioni ya
fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Alikabidhiwa tuzo hiyo jana ikiwa imepita takriban mwaka mmoja tangu
aibue bungeni kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power
Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200
kifisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Kashfa ya akaunti hiyo ilihusisha baadhi ya maofisa waandamizi wa
serikali, wakiwamo mawaziri, katibu mkuu wa wizara, aliyekuwa
mwanasheria mkuu wa serikali (AG), viongozi wa dini na majaji.
Mbali na Kafulila, wengine waliotunukiwa tuzo kama hiyo, ni pamoja na
waliokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK); Salma Said na Adil
Mohamed.
‘Wajumbe’ hao walitunukiwa tuzo hiyo kutokana na kuwa kati ya watu
waliokuwa wakifuatiliwa na mtu asiyefahamika kutokana na kutuhumiwa
kuipigia kura ya hapana katiba inayopendekezwa katika Bunge hilo.
Mwingine aliyetunukiwa tuzo kama hiyo ni Mkurugenzi wa Taasisi ya
Wafugaji Wanawake Loliondo, Maanda Ngoitick, ambaye alifikia
kudhalilishwa kwa kuitwa kuwa siyo raia wakati akiwatetea wanawake wa
jamii hiyo.
Tuzo hizo zilizo andaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
(THRDC) zilitolewa katika maadhimisho ya Siku ya Watetezi wa Haki za
Binadamu Duniani, jijini Dar es Salaam jana.
Harakati zao hizo zimetambuliwa na Ripoti ya Hali ya Watetezi wa Haki
za Binadamu Tanzania ya Mwaka 2014 iliyotolewa na THRDC jana.
Katika maadhimisho hayo, maonyesho ya mashirika, taasisi, wadau,
watetezi, wanaharakati, kikiwamo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Jukwaa la Katiba (Jukata) na Jumuiya ya Ulaya (EU) na Chama cha
Albino Tanzania (TAS), yalizinduliwa.
Mgeni rasmi katika maadhimisho alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, Tom Bahame Bahame, ambaye alisema tume yake
imejipanga kuzishirikisha taasisi mbalimbali katika kuhakikisha maadili
ya uongozi yanafuatwa.
Alisema pia itahakikisha haki ya kujiandikisha katika Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura na ushiriki wa wananchi katika mchakato wa upigaji
kura katika uchaguzi mkuu, mwaka huu.
Chanzo: NIPASHE
Comments