Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi amesema anahofia
usalama wa maisha yake, kufuatia habari iliyoandikwa katika gazeti moja
la kila wiki kwamba, Rais Jakaya Kikwete aliapa kupambana naye jambo
ambalo limempa hofu kubwa.
Kadhalika, amelalamikia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya
Habari Maelezo kwa kukaa kimya na kuacha kutoa ufafanuzi dhidi ya tuhuma
hizo, huku taarifa hizo zikiendelea kusambazwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mengi
alisema kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake kuwa yeye ni kinara wa
kuhujumu serikali ya Rais Kikwete siyo za kweli.
Dk. Mengi alisema amesoma kwa masikitiko makubwa habari
iliyochapishwa Machi 23, mwaka huu na gazeti la Taifa Imara, yenye
kichwa cha habari ‘Zitto amchongea Mengi kwa JK’ ambapo pamoja na mambo
mengine inasema kuwa Zitto Kabwe amemchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete
kwamba ndiye kinara wa kuhujumu serikali yake.
Alisema habari hiyo ambayo chanzo chake kimeelezwa kwamba ni Ikulu,
iliendelea kueleza kuwa Zitto alikutana na Rais Kikwete muda mfupi baada
ya kuwasilisha bungeni ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) kuhusiana na kashfa ya Escrow ambayo Zitto alikuwa ni mwenyekiti
wake.
“Habari hiyo inasema kwamba katika mazungumzo yake na Rais Kikwete
Zitto amenukuliwa akimueleza mkuu huyo wa nchi kuwa anayesababisha
serikali yake iyumbe kila mara ni Mengi,” alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi alisema habari hiyo ambayo nakala yake ameiambatanisha
kwenye taarifa yake, inasema yeye Zitto , binafsi amekuwa akishawishiwa
na Dk. Mengi kuiangusha serikali ya Rais Kikwete.
Hata hivyo, Dk. Mengi alisema katika habari hiyo Zitto alikwenda
mbali zaidi kumueleza Rais Kikwete kuwa Dk. Mengi ameapa kuwa Rais
Kikwete akimaliza muda wake wa Urais atamshughulikia kwa nguvu zake
zote.
Alisema habari hiyo imeeleza kwamba baada ya maelezo hayo, Rais
Kikwete aliapa kupambana na Dk. Mengi na akamshukuru Zitto kwa kumpa
taarifa hizo.
Mengi alisema tuhuma zilizotolewa kuhusu nia yake ya kutaka
kuiangusha serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza
muda wake wa uongozi, zimemshtua sana na tamko la kwamba Rais Kikwete
aliapa kuwa atapambana na yeye zimempa hofu kuhusu mustakabali wa maisha
yake.
Alisema kuwa hofu yake kubwa inasababishwa na Ikulu na Idara ya
habari Maelezo kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi
wowote.
“Najua umakini wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya habari
Maelezo katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote linalomhusu
Rais, lakini katika hili nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua kukaa
kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa,”alisema Dk. Mengi.
Aliongezea kusema kuwa,” hofu yangu inazidi kuwa kubwa kwa sababu
Rais ni Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama. Kauli yake kama
ilivyonukuliwa na gazeti hili kwamba atapambana na mimi inawezekana
kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo vya dola kuniangamiza,” alisema.
Alitolea mfano mwaka 1170, Askofu Mkuu wa Canterbury nchini Uingereza
aliuawa baada ya walinzi wa mfalme kusikia mfalme akisema “hakuna
anayeweza kuniondolea huyo mkorofi?”. Walinzi wake wakadhani mfalme
ameagiza wamuue Askofu huyo na wakamuua, alisema.
Chanzo: NIPASHE
Comments