Wabunge wa chama kikuu cha Upinzani Tanzania Chadema, Saed Kubenea
(Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) leo Alhamisi Oktoba 18, 2018
wamevuliwa nafasi zao za uongozi.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika ametangaza uamuzi huo leo
katika mkutano na waandishi wa habari ambao wabunge hao waliutumia
kuomba radhi juu ya mpango wao hasi dhidi ya Meya wa Ubungo, Boniface
Jacob wakibainisha hawakuwa na nia Mnyika alikuwa akisoma maazimio ya kikao cha kamati kuu kilichowahoji wabunge hao jana Jumatano Oktoba 17, 2018.
Amesema wabunge hao pia wamevulia uongozi ndani ya chama hicho huku wakiwekwa kwenye kipindi cha uangalizi wa miezi 12.
Kubenea
na Komu katika siku za hivi karibuni wamezua mjadala ndani na nje ya
chama hicho kwa kile kinachodaiwa kuwa ni sauti yao iliyokuwa ikisikika
wakipanga mpango hasi dhidi ya Jacob.
Wabunge hao kwa nyakati
tofauti wamekana kuhusika na sauti hizo kwa kile walichoeleza ni za
kutengeneza huku Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo (Chadema) naye
akieleza kupeleka suala hilo ndani ya chama.
Lakini leo wamekiri kuwa sauti hizo ni zao na kuomba radhi wakibainisha kuwa hawakuwa na nia ovu.
Akisoma
maazimio ya kamati kuu Mnyika amesema, “kamati kuu iliitishwa na
ikafanya kikao chake juu ya tuhuma za utovu wa nidhamu wa wabunge hawa.”
“Baada
ya kuhojiwa hatimaye kamati kuu ilifikia uamuzi na kuwakuta na hatia ya
ukiukwaji wa kanuni na maadili ya chama. Imewapa onyo kali kuwataka
waandike barua ya kuomba radhi kwa chama na kwa watajwa kufuatia maneno
yaliyozungumzwa.”
Akizungumza baada ya Mnyika kumaliza kusoma
maazimio hayo, Kubenea amesema, “kama ambavyo mmelezwa nichukue nafasi
hii kusema kwamba yaliyotokea siku hiyo ni bahati mbaya na hatukuwa na
nia yoyote ovu kwa msingi huo naomba radhi wote walioguswa na watanzania
kwa jumla.”
Kwa upande wake Komu amesema, “nichukue nafasi hii
kwanza kwa kukishukuru chama kwa jinsi ilivyolichukulia jambo hili na
kulipa uzito.”
“Chama ni kikubwa kuliko sisi wote na sisi ni
vyombo vya chama, chama kina mikono yake. Kwa kutambua sisi ni vyombo
vya chama tunatekeleza maagizo na tayari tumeshaandika barua za kuomba
radhi.”
Komu amesema, “tunaomba radhi watanzania yale mazungumzo
yetu yalikuwa ya faragha ila teknolojia ikatuzidi yakasambaa unajua
mnavyokuwa kwenye faragha mnajiachia. Kwa hayo yaliyotokea tunaomba
radhi, tunataka kuanza ukurasa mpya bila kuwa na kigugumizi.”
Comments