Marekani imeomba Uturuki kutoa
ushahidi wa kanda ya sauti inayodai kuwa mwanahabari wa Saudi Arabia
Jamal Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul.
Rais Trump amewaambia waandishi katika ikulu ya White House kuwa,
“Tumeomba kupewa nakala kanda hiyo, kama ni kweli ipo,”.
Bwana
Khashoggi hajawahi kuonekana tangu alipoingia jengo la ubalozi wa Saudi
Arabia tarehe mbili mwezi huu wa Oktoba. Saudi Arabia amekanusha madai
yakuhusika na kutoweka kwa mwandishi huyo.
Huku hayo yakijiri,
Gazeti la Washington Post limechapisha makala ya mwisho yaliyoandikwa na
bwana Khashoggi kabla ya kutoweka kwake. Katika makala hayo
anazungumzia umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari katika eneo la
Mashariki ya kati.
Mhariri wa kimataifa wa gazeti hilo Karen
Attiah amesema uchapishaji wa makala hayo ulisitishwa kwa ajili ya kuwa
na matumaini kwamba bwana Khashoggi atarejea salama. Aliandika akisema
“Sasa sina budi kukubali: Kwamba hilo halitafanyika. Hii ndio makala
yake ya mwisho nitakayosahihisha”.
Bi
Attiah pia aliongezea kusema, “Makala haya yanaangazia kwa kina
kujitolea kwake kupigania uhuru katika mataifa. Uhuru ambao alipigania
kwa maisha yake.”
Kuwepo kwa ushahidi kwamba bwana Khashoggi –
mkosoaji mkuu wa viongozi wa Saudi – aliuawa kulifichuliwa na wachunguzi
wa Uturuki. Ripoti katika vyombo vya habari vya taifa hilo zinaelezea
taarifa za kutisha za dakika za mwisho za mwandishi huyo. Gazeti moja la
Uturuki linasema sauti ya balozi wa Saudi Arabia mwenyewe Mohammed al
Otaibi inasikika katika kanda hiyo iliyonasa kifo cha bwana Khashoggi.
Yeni
Safak, ambayo ina uhusianaop wa karibu na serikali imemnukuu balozi
huyo akidai kuwa Saudia ilituma maajenti mjini Istanbul: “Msiseme hili.
Mtanitia mashakani.”
Bwana Otaibi alirejea mjini Riyadh siku ya Jumanne.
Saudi
Arabia ni moja ya washirika wa karibu wa Washington na kupotea kwa
Khashoggi kumeiweka utawala huo katika hali ya kutatanisha. Akigusia
sauti iliyorekodiwa na ambayo inadaiwa kuwa na ushahidi wa mauaji ya
Khashoggi ,Trump aliongeza: “Sina uhakika ya kuwepo kwa sauti hiyo,
lakini huenda ikawa ni kweli ipo.”
Bwana Trump amesema anatarajia
ripoti kutoka kwa waziri wa wake wa mambo ya nje Mike Pompeo ambaye
alikua nchini Saudi Arabia na Uturuki. Rais Trump amesema ukweli
kuhusiana na suala hilo utajulikana “Kufikia mwisho wa wiki”.
Amekanusha madai kwamba anajaribu kusaidia Saudi Arabia kutakasa jina
lake: “Hapana, hilo haliwezekani, Kile ninachofanya ni kufahamu kile
kinachoendelea.”
Katika kipindi cha siku chache zilizopita Trump
amegusia uwezekano wa “Wauaji katili” kuhusika na kutoweka kwa mwandishi
Jamal Khashoggi. Pia aliwaomba watu kutokimbia kuwalaumu viongozi wa
Saudia kabla ya kuthibitisha kuhusika kwa viongozi hao katika kisa hiki.
Kwa
mujibu wa shirika la habari la Reuters, siku ya Jumatano na Alhamisi,
kundi la maafisa wa wachungizi wa Uturuki walipekua makaazi ya balozi wa
Saudi Arabia mjini Istanbul kwa karibu saa tisa na baadae kuelekea
katika jengo la ubalozi lililopo mita 200 kutoka makaazi hayo.
Kundi
hilo la wachunguzi lilihusisha viongozi wa mashtaka pamoja na watalamu
wa upasuaji waliokuwa wamevalia mavazi meupe. Magari kadhaa ya Saudia
yaliyo na nambari ya usajili ya kidiplomasia yalinaswa katika picha ya
CCTV yakiingia makaazi ya balozi chini ya saa mbili baada ya bwana
Khashoggi kuingia ubalozi huo siku alipotoweka.
Ubalozi huo
ulipekuliwa kwa mara ya kwanza siku ya Jumatatu. Siku ya Jumanne waziri
wa mambo ya nje wa Marekani alisafiri mjini Riyadh kufanya mazungumzo na
mfalme Salman wa Saudi Arabia na mwanamfalme Mohammed bin Salman,
ambaye amekanusha vikali kuhusika kwake na kotoweka kwa mwanahabari
Jamal Khashoggi.
Chanzo BBC
Comments