Huzuni na Simanzi zimetawala katika viwanja vya Manispaa ya Kinondoni leo katika kuaga Mwili wa aliyekuwa diwani wa Kata ya Magomeni kwa kipindi cha miaka kumi na nne(14), Mh.Juliani Rushaigo Bujugo aliyefariki juzi juzi jijini Dar es Salaam.
Akiongoza shughuli hiyo iliyohudhuriwa pia na viongozi wa vyama na Serkali, Mstahiki Meya wa Manispaa ya kinondoni Mh.Benjamini Sitta amesema, Kinondoni imepoteza mpiganaji, mpenda haki, mtetezi wa wanyonge, na mzalendo.
"Bujugo alikuwa mzalendo, alikuwa ni mtu aliyependa kuona mambo yanakwenda, wanyonge wanapata haki, hata siku ambayo usiku wake mauti inamkuta, Mh Bujugo alikuja ofisini kwangu mchana kwa swala la walemavu wa magomeni kuhusiana na ada ya usajili wa kikundi wanayotozwa" Alisema Meya Sitta.
Shughuli hii ya kuuaga mwili wa marehemu Julian Rushaigo Bujugo imehudhuriwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Ndg Aron Kagurumjuli, wakuu wa idara na vitengo, wananchi wa kata ya Magomeni, pamoja na viongozi wa vyama na serikali, akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Bi.Kate Kamba, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni Ndg. Harold Maruma, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh Paul Makonda, pamoja na Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni.
Bwana ametoa, bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.
Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi Amen.
Comments