Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani nchini fanya ziara ya kushtukiza kwenye Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (Udart)
Kamanda wa Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani nchini , Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Fortunatus Musilimu amefanya ziara ya kushtukiza kwenye barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (Udart) pamoja na Kituo cha Kimara Mwisho cha mabasi hayo na kujionea baadhi ya kero zinazowakumba abiria wa kituo hicho.
Kamanda, Musilimu akiwa na msafara wake alianzia ziara hiyo kwa kuanzia katikati ya mji na kuelekea moja kwa moja kwenye kituo hicho, ambapo msafara huo ukiwa eneo la Jangwani ulibaini madereva wa mabasi kuendesha kwa ziadi ya mwendo wa Kilomita 60 wakati sheria inawataka waendeshe chini ya kilomita 50.
Kupitia chombo maalum cha kupima mwendo walibaini moja ya mabasi hayo kukiuka sheria hiyo katika eneo hilo liliopita kwa kasi hiyo.
Msafara huo ukiwa unakaribia eneo la Magomeni ulibaini pia baadhi ya magari ya kawaida kuvunja sheria za usalama barabarani kwa kutumia barabara ya mradi wa mabasi hayo.
Kamanda wa kikosi hicho (SACP), Musilimu akiwa katika Kituo cha Kimara Mwisho ilimchukua muda mrefu kuangalia huduma ya usafiri inavyotolewa na Udart kupitia abiria waliokuwa wakielekea Kivukoni na Gerezani, akiwa kituoni alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya abiria waliomueleza kero zao.
Mmoja wa abiria aliyekuwa akielekea Kivukoni, Poza Hassan alimuelezea kamanda huyo kuwa hali huwa ngumu nyakati za asubuhi ambapo abiria hupata adha kubwa wakati wa kupanda mabasi hayo.
“ Kiukweli kwa mtu wa kawaida ni kero kutumia usafiri huu kwani mrundikano wa abiria ni mkubwa hali inayoonyesha mabasi ni machache wakati wa asubuhi kusababisha watu kukanyagana na kupoteza mali zao,” alisema Poza.
Alisema wakati wa jioni abiria wanaotoka mjini kurudi nyumbani kwao hukumbana na adha ya aina hiyo hiyo ya kugombania mabasi hayo na kuwa pendekezo lake wahusika wafanye utafiti na kupata data ambazo sio za kupika ili kupata majawabu juu ya kero hizo.
Kwa upande wake, abiria Richard Msuya alibainisha kuwepo kero hiyo kila siku huku akisisitiza kuwepo mbadala wa mabasi mengine ya makampuni mengine ili kuleta ushindani utakaosababisha kuondoa adha hiyo.
“ Mkuu naona hawa jamaa wanafanya hivi sababu hakuna ushindani wapo wenyewe tu kungekuwa na mabasi ya watu wengine yanayoleta ushindani kero zisingekuwepo ni bora warudishe daladala kama zamani ziwaletee changamoto,” alisema Msuya.
Baada ya kusikiliza kero hizo Kamanda na msafara wake aliamua kukagaua baadhi ya mabasi hayo na kubaini makosa mbalimbali ambapo katika basi lenye namba T 109 lilikutwa na kosa kutokuwa na matairi imara likatozwa faini na dereva, William Kasonzo kuagizwa kulirudisha yadi.
Gari jingine lenye namba T 997 DGV liliokuwa linaendeshwa na dereva, Adelaida Nyasi lilibainika kukutwa na faini ya muda mrefu ambayo ilikuwa haijalipwa.
Kamanda, Musilimu baada ya kujionea kero katika ziara aliyoifanya kwa kushtukiza aliagiza uongozi wa Udart kuyashughulikia matatizo hayo yaliyobainishwa na wananchi pamoja na aliyojionea.
“ Nimeshuhudia madereva wanavyoendesha kwa kasi Jangwani hata magari ya abiria kuingia kwenye barabara ya Udart , nachoweza kusema tukimkamata dereva wa namna hiyo tunamfungia leseni yake,” alisema.
Aliongeza kusema kuwa ndani ya mabasi hayo wamebaini kutokuwepo mikanda ya kutosha ya kushikia abiria waliosimama na kukazia watakuwa wakali kwa kutumia staili ya nyakua nyakua.
Naye, Mmoja wa maofisa wa Udart, Joe Beda aliyepewa maelekezo hayo alisema atayafikisha kwa uongozi wa juu ili yatafutiwe ufumbuzi.
Comments