Ubelgiji imetakiwa kuongeza kiwango cha uwekezaji nchini ili kuchochea zaidi kasi ya azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kauli hiyo ilitolewa leo na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mhandisi Stella Manyanya (Mb) alipokuwa anatoa hotuba ya ufunguzi wa Kongamano la Wafanyabiashara wa Ubelgiji na Tanzania linalofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar Es Salaam.
“Kuna miradi 32 yenye thamanai ya Euro milioni 902 ambayo imeajiri wafanyakazi 1814 inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Ubelgiji nchini Tanzania. Hivyo, kuna umuhimu wa kuongeza uwekezaji huo kwa kuwa mazingira ya uwekezaji nchini ni mazuri na yanavutia”, Mhandisi Manyanya alisema.
Mhe. Naibu Waziri aliwahamiza wawekezaji hao ambao ni wafanyabiashara wakubwa nchini Ubelgiji kuwekeza katika sekta za kilimo, hususan kwenye maeneo ya viwanda vya nguo, sukari, mafuta ya kupikia, maziwa, ngozi, nyama, mbegu, matunda na maua,
Sekta nyingine aliyoitaja ni ya nishati hasa katika miundombinu ya kuzalisha na kusambaza gesi asilia na nishati jadilifu.
Maeneo mengine yaliyosisitizwa na Mhe. Naibu Waziri ni pamoja na sekta ya utalii, madini, uvuvi katika bahari kuu, miundombinu, maeneo maalum ya viwanda (industrial parks) na ujenzi wa majengo hususan katika mji mkuu wa Dodoma ambapo mahitaji ni makubwa.
Uzalishaji wa dawa za binadamu na wanyama, vifaa tiba na uzalishaji wa samani za kisasa ni maeneo ambayo Mhe. Naibu Waziri aliwasihi wawekezaji hao kuyapa jicho la pekee.
Mhe Manyanya alisema wawekezaji watakaoamua kuwekeza nchini hawatajutia uamuzi wao kwa kuwa Tanzania kuna mazingira mazuri. Mazingira hayo ni pamoja na amani na usalama, rasilimali za kutosha na uhakika wa soko kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na hatua zinakamilishwa kuwa na eneo huru la biashara barani Afrika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kukuza Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. John Mathew Mnali aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa TIC itatoa msaada unaohitajika kupitia kituo chake cha kutoa huduma kwa pamoja (One Stop Centre) kwa mfanyabiashara yeyote mwenye dhamira ya kuwekeza nchini. Alitaja msaada wanaotoa kupitia kituo hicho ni pamoja na msaada wa kupata vibali vya kazi na makazi, kupata ardhi ya kuwekeza, miongozo ya kodi ikiwemo kupata Namba ya Utambulisho ya Mlipa Kodi (TIN), kuthibitisha bidhaa kutoka Shirika la Viwango Tanzania, Mamlaka ya Chakula na Dawa na masuala ya kupata vibali vya mazingira (environment clearance).
Bw. Mnali alibainisha kuwa kuna bandari kubwa tatu nchini zinaunganisha nchi jirani ambazo hazina bandari. Aidha, Tanzania inaongoza kikanda kupokea miradi ya moja kwa moja ya uwekezaji kutoka nje (FDI) na pia ni miogoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi duniani. Alisema sababu hizo ni vigezo tosha vya kuichagua Tanzania kuwa kimbilio la uwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Wafanyabiashara la Umoja wa Ulaya nchini, Bi. Marie Strain alisema kuwa nchi za umoja huo zinashika nafasi ya pili kwa kufanya biashara na Tanzania. Hivyo kundi hilo linatoa huduma mbalimbali kwa Wafanyabiashara zikiwemo za ushauri, taarifa za masoko na maeneo ya uwekezaji pamoja na kufanya majadiliano na Serikali namna ya kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji.
Katika mahojiano na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Jestas Nyamanga alisema kuwa ujio wa wawekezaji hao unatokana na juhudi za Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji za kuvutia wawekezaji. Alisema Ubalozi umefanya hivyo, huku ukitambua kuwa takwimu zinaonesha kuwa Ubelgiji ni moja ya nchi kumi duniani zinazoongoza kwa kufanya uwekezaji nje ya nchi.
Comments