Wakazi wa kisiwa cha Anjouan nchini Comoro wamesema kumekuwa na milio ya risasi katika mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo Mutsamudu, baada ya vikosi vya ulinzi kuvunja vizuizi vya barabarani, ambapo serikali inasema viliwekwa na upinzani.
Kwa mujibu wa BBC Swahili, Waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo Mohamed Daoudou amewalaumu waandamanaji kwa kutumia silaha za moto na kupinga kuwa askari wake ndiyo waliofyatua risasi.
Amesema kuwa gavana wa Anjouan Abdou Salami Abdou ambaye ni mwanachama wa upinzani ndiye aliyepanga na kusababisha machafuko hayo.
Kumekuwa na maandamano na wandamanaji wengi kukamatwa katika kisiwa hicho chenye mkusanyiko wa visiwa vingi katika bahari ya Hindi tangu Julai mwaka huu baada ya Rais wa nchi hiyo Azali Assoumani kushinda uchaguzi wa kura ya maoni yenye utata na kumaliza utamaduni wa kuongoza kwa mzunguko katika nchi hiyo yenye visiwa vikubwa vitatu na kumfanya rais huyo kuendelea kusalia madarakani.
Comments