Na Victor Melkizedeck Abuso
Wataalam wa Umoja wa Mataifa wanazuru Rwanda siku kadhaa baada ya
Marekani kuiwekea serikali ya Kigali vikwazo kutokana na waasi wa M 23
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwatumia watoto katika
jeshi lake, waasi ambao Rwanda inatuhumiwa kuwaunga mkono.
Wakaazi wa Mashariki mwa DRC wakikimbia makwao
Rais Paul Kagame anakutana na wataalam hao ambao pia walizuru mji wa
Goma kuthathmini hali ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo, kipindi hiki
Kigali ikiendelea kukanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M 23 au
kujihusisha na machafuko nchini DRC.
Wiki iliyopita, serikali ya Marekani ilitangaza kuiwekea vikwazo
serikali ya Kigali kwa kusitisha mafunzo na ufadhili wa jeshi lake baada
ya ripoti ya umoja wa Mataifa kuonesha kuwa Kigali imeedelea kuwaunga
mkono waasi wa M 23 wanaotumia watoto katika jeshi lake.
Tuhuma za utumizi wa watoto katika jeshi la M 23 zimekanushwa vikali na
kiongozi wa kundi hilo Betrand Bissimwa ambaye ameiambia RFI Kiswahili
kuwa sheria zao haziruhusu watoto kutumiwa katika jeshi lake na madai
hayo hayo hayana msingi.
Katika hatua nyingine, Umoja wa Mataifa unasema utulivu Mashariki mwa
DRC unaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo ya kisiasa wala sio
matumizi ya nguvu.
Alexis Lamek, Naibu Balozi wa Ufaransa katika Umoja huo amesema kuwa
mazungumzo ndio njia ya pekee kwa sababu waasi wa M 23 tayari walikuwa
wamejumuishwa katika jeshi la serikali mwaka 2009 baada ya muafaka wa
amani.
Comments