Arusha. Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, amepinga
uamuzi wa kusimamishwa kwa maelezo kuwa kikao kilichochukua uamuzi huo
hakitambuliki kikatiba huku akikanusha tuhuma za kutumiwa na Naibu
Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, kukisambaratisha chama hicho.
Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto
nimekuwa nikizisikia, lakini huo ni upofu, mimi si mtu wa kutumika nina
elimu yangu nzuri ya shahada ya kwanza ya utawala wa biashara, najua
ninachokifanya ni kwa masilahi ya chama. Samson Mwigamba
Akizungumza jana na gazeti hili, Mwigamba alisema kikao ambacho kina
mamlaka ya kumwajibisha ni Kamati Kuu baada ya kupokea tuhuma na
kumsikiliza.
“Baraza la uongozi la Kanda halina mamlaka ya kunisimamisha uenyekiti,
lakini kwa kuwa mimi bado ni mwanachama hai wa Chadema na sitahama
Chadema, nitakaa pembeni ili chama kifanye uchunguzi wa tuhuma zangu
nikiwa nje ya ofisi,” alisema Mwigamba.
Hata hivyo, alisema anakusudia kufafanua chanzo cha mgogoro wake na
baadhi ya viongozi leo, baada ya kukabidhiwa kompyuta mpakato (laptop)
na viongozi wa chama hicho ambao waliichukua ili kuifanyia uchunguzi.
Akana kutumiwa na Zitto
Akizungumzia tuhuma za muda mrefu kuwa, amekuwa akitumiwa na Zitto hasa
kuelekea uchaguzi ndani ya chama hicho, alisema wanaofikiri hivyo ni
vipofu wa kisiasa.
“Hizi tuhuma kuwa natumiwa na Zitto nimekuwa nikizisikia, lakini huo ni
upofu, mimi si mtu wa kutumika nina elimu yangu nzuri ya shahada ya
kwanza ya utawala wa biashara, najua ninachokifanya ni kwa masilahi ya
chama,” alisema Mwigamba.
Comments