LOS ANGELES, Marekani
MIEZI michache baada ya kufunga ndoa kwa siri na bilionea wa Qatar, mwanamuziki nyota wa Marekani, Janet Jackson amepanga kuasili mtoto ili kuongeza familia yake.
Janet, ambaye ni dada wa mwanamuziki nyota wa zamani wa miondoko ya pop duniani, Michael Jackson, anataka kuasili mtoto huyo aidha Jordan au Syria.
Chanzo cha habari kimelieleza gazeti la US Weekly la Marekani juzi kuwa, Janet (47) ameshaanza kufanya taratibu za kuasili mtoto kutoka nchi za dunia ya tatu.
Janet alifunga ndoa na mfanyabiashara huyo, Wissam Al Mana hivi karibuni, lakini ndoa hiyo ilifanywa kuwa siri kubwa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, Janet anataka kuasili mtoto kwa vile si rahisi kwake kupata uja uzito kwa sasa.
"Ndio sababu ameamua kuasili mtoto. Katika kipindi hiki, ambacho anaishi nje ya Marekani, amekuwa akiguswa sana na matukio yanayotokea katika nchi za Syria na Jordan,"kimesema chanzo hicho cha habari.
Kiliongeza kuwa, bado haijajulikana ni lini mwanamuziki huyo atakamilisha taratibu hizo, lakini tayari ameshaanza kuzifanya.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la US Weekly, Janet ameomba msaada wa Malkia Rania wa Jordan ili aweze kukamilisha mpango wake huo.
Gazeti hilo limeongeza kuwa, Janet ana hamu ya kuanzisha familia na Al Mana, ambaye walianzisha uhusiano wa kimapenzi tangu 2010.
"Anataka watoto. Kama hawezi kuwapata, ataasili,"kimesema chanzo hicho cha habari.
Al Mana ni mume wa tatu wa Janet. Awali, aliolewa na James DeBarge na Rene Elizondo. Pia alikuwa na uhusiano wa muda mrefu na Jermaine Dupri.
Comments