Na Victor Melkizedeck Abuso
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana siku ya Jumatatu
kuzungumzia mapigano mapya yanayoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo kati ya waasi wa M 23 na majeshi ya serikali
yakisaidiwa na yale ya Umoja wa Mataifa.
Kuendelea kwa mapigano hayo kumeisukuma Ufaransa kuitisha kikao hicho
cha dharura huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akishtumu
mapambano yanayoendelea.
Kikao hicho kitafanyika huku jeshi la serikali likifanikiwa kuchukua
uthibiti wa ngome za M 23 katika miji ya Rutshuru na Kiwanja.
Mapambano hayo yalianza wiki iliyopita baada ya mazungumzo ya amani kati
ya waasi hao na serikali ya DRC kukwama jijini Kampala Uganda, na
yamesababisha maelfu ya waakazi wa Mashariki kukimbia makwao na
kusababisha kuuawa kwa mwanajeshi mmoja wa Umoja wa Mataifa kutoka
nchini Tanzania.
Kiongozi wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa MONUSCO Martin
Kobler amesema kuwa mwanajeshi huyo wa Tanzania aliuawa wakati
akiwalinda raia katika mji wa Kiwanja na anakuwa mwanajeshi wa tatu
kutoka nchini Tanzania kuuawa katika mapambano hayo.
Msemaji wa jeshi la Serikali Mashariki mwa nchi hiyo Kanali Olivier
Hamuli, ameimbia RFI Kiswahili kuwa vikosi vya serikali vimefanikiwa
pakubwa kuwarudisha waasi wa M 23 na sasa wanathibiti miji ya Rutshuru
na Kiwanja.
Comments