YANGA jana ilichupa nafasi za juu katika msimamo wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ilikuwa na ushindani mkali kutokana na kila timu kuonyesha kandanda ya kiwango cha juu.
Matokeo hayo yameiwezesha Yanga kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi saba, nyuma ya Simba inayoongoza kwa kuwa na pointi 15.
Mshambuliaji Mrisho Ngasa aliiandikia Yanga bao la kwanza dakika ya saba baada ya kupokea pasi kutoka kwa Didier Kavumbagu na kufumua shuti lililompita kipa Hussein Sharrifu na mpira kutinga wavuni.
Baada ya kufunga bao hilo, Ngasa alikwenda kwenye jukwaa linalokaliwa na mashabiki wa Simba na kuwaonyesha ishara za kuwadhihaki.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Kavumbagu dakika ya 24 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Ngasa, aliyemtoka beki Paul Ngelema wa Mtibwa.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Prisons iliichapa Mgambo JKT bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.Inatoka kwa mdau.
Comments