NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, amesema anatafakari upya uamuzi wake wa kuachana na siasa baada ya kushuhudia hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi wa mkoa wa Tabora.
Alisema
kutokana na hali duni ya maisha ya wananchi aliyoishuhudia katika
maeneo mbalimbali kwenye majimbo ya Sikonge na Igalula, atahakikisha
kwa kushirikiana na viongozi wenzake ndani ya CHADEMA wanakifuta Chama
cha Mapinduzi (CCM) katika Kanda ya Magharibi.
Zitto
ambaye alikwishakutangaza kutogombea tena ubunge katika Jimbo lake la
Kigoma Kaskazini kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, alitoa kauli hiyo juzi
katika mikutano ya hadhara, katika majimbo ya Sikonge na Igalula, ukiwa
ni mwendelezo wa ziara yake ya ujenzi wa chama katika kanda hiyo.
Maeneo
aliyoyatembelea na kukuta hali ya wananchi ikiwa hairidhishi hususan
katika kupata huduma ya maji ni kata za Ipole, Kitunda na Sikonge,
zilizo jimboni Sikonge na kata za Miswaki, Kigwa na Loya zilizoko
Igalula, wilayani Uyui.
Alisema
kuwa licha ya wabunge wa mkoa huo kutokana na chama kinachotawala kwa
zaidi ya miaka 50, wamekosa sauti ya kuzungumzia matatizo ya wananchi
kwa sababu ya kulinda masilahi binafsi.
Zitto
alifafanua kuwa ni jambo la kusikitisha kuona mikoa ya magharibi ikiwa
nyuma kimaendeleo licha ya kuchangia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni
katika pato la taifa kupitia kilimo cha tumbaku.
"Ninatafakari
upya uamuzi wangu wa kuachana na siasa, ni vigumu kama sitashirikiana
na wenzangu kuhakikisha hali hii ya watu kugombea maji ya kunywa na
wanyama katika shimo moja inakwisha," alisema.
Aliwataka
wananchi wawaunge mkono pale wanapopambana bungeni hata ikibidi kupanda
juu ya meza au kutoka nje pindi masilahi ya watu yanapopuuzwa, kwa
sababu ya kuwapo kwa wabunge wengi wa CCM ndani ya Bunge.
Zitto
aliongeza kuwa serikali ya CCM imechoka na haiwezi kuongoza na kwamba
kama ilishindwa kusimamia reli iliyojengwa na wakoloni haiwezi kuongoza
nchi iliyogubikwa na umaskini licha ya kuwa na utajiri kila sehemu.
"Laiti
kama mngejua yale tunayoyajua na kuyapigania bungeni hususan ufisadi
unaofanywa na serikali ya CCM, naamini wananchi mngeingia barabarani
kuhakikisha serikali hii inatoka madarakani," alisisitiza.
Akizungumzia
uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa vyama vya
CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kujadili muswada wa sheria wa Katiba,
Zitto alisema ni wazi amedhihirisha kwamba Waziri Stephen Wassira
alikuwa akiongea kitu ambacho hakijui.
Alisema
wakati wapinzani walipotoka bungeni kupinga muswada huo, Wassira
alisimama hadharani na kusema kwamba wapinzani hawatapata fursa
nyingine ya kujadiliana na Ikulu kuhusu Katiba.
Akiwa
katika Kata ya Loya, Jimbo la Igalula, Zitto alisema kitendo cha
serikali kuwanyanyasa wafugaji ni udhalilishaji dhidi ya utu, kwa kuwa
kila Mtanzania ana haki ya kuishi sehemu yoyote ili mradi asivunje
sheria.
Alisema
viongozi wa CCM wamekuwa wakiwatumia wafugaji kama mifuko yao ya
hifadhi, kwa kujipatia fedha kinyume cha sheria, hali aliyoelezea kuwa
ni ukiukaji wa utawala bora.
Zitto alieleza kusikitishwa na
taarifa ya walimu wa Kata ya Loya kuwa wanatumia sh 20,000 kwa ajili ya
kuweza kufika barabara kuu ya kuelekea mjini Tabora kufuatilia
mishahara yao.CHANZO TANZANIA DAIMA.
Comments