LONDON, England
KLABU ya Manchester United ya England, imempa mshambuliaji wake chipukizi, Adnan Januzaj ofa ya mshahara wa pauni 60,000 za Uingereza (sh. milioni 138) kwa wiki ili abaki katika klabu hiyo.
Uamuzi huo wa Manchester United umekuja siku chache baada ya chipukizi huyo wa kimataifa wa Ubelgiji, kufunga mabao mawili katika mechi ya ligi dhidi ya Sunderland iliyochezwa kwenye uwanja wa Light.
Januzaj (18), ambaye ni zao lingine la kizazi kipya cha Ubelgiji, alifunga mabao hayo mawili baada ya Manchester United kuwa nyuma kwa bao 1-0. Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Januzaj kucheza kwa dakika 90 katika ligi kuu ya England.
Mkataba wa chipukizi huyo kuichezea Manchester United, unatarajiwa kumalizika miezi minane ijayo na tayari klabu kadhaa za Ulaya, zikiwemo Manchester City, Real Madrid na Chelsea zimeshaanza kumtolea macho.
Kocha Mkuu wa Manchester United, David Moyes amesema atahakikisha anampa Januzaj mkataba mpya ili abaki katika klabu hiyo.
Staili ya uchezaji anayotumia chipukizi huyo wa Ubelgiji, inafanana na ile ya Wayne Rooney wakati alipokuwa akiichezea Everton kabla ya kunyakuliwa na Manchester United.
"Anajiamini sana,"alisema Rooney. "Vijana wengi wanaochipukia hivi sasa hawajiamini na waoga, lakini anaonekana kuifurahia kazi yake, anajiamini na uwezo wake ni mkubwa. Ni aina ya mchezaji, ambaye kila kocha angependa kuwa naye."
"Anamiliki mpira vizuri, anakimbia na mpira kumwendea adui. Nafikiri kocha amefanya jambo zuri kumjumuisha kwenye kikosi, hasa kutokana na yaliyotokea katika mechi chache zilizopita,"aliongeza Rooney, alipokuwa akimzungumzia chipukizi huyo.
Rooney pia alimtetea Moyes, akisisitisa kuwa hapaswi kulaumiwa kutokana na kufanya vibaya kwa timu hiyo katika ligi. "Amekuja kocha mpya na bado hatujaweza kucheza vizuri. Tunajua ni sisi tunaomuangusha,"alisema.
Mabao ya Januzaj pia yalipunguza presha iliyokuwa ikimkabili Moyes kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuvurunda katika mechi za hivi karibuni.
Moyes ni muumini mkubwa wa vijana wenye vipaji na ndiye aliyemwibua Rooney na kumpa nafasi kwenye kikosi cha Everton. Moyes pia ndiye aliyemwibua chipukizi mwingine wa Manchester United, Ross Barkley katika siku za hivi karibuni.
Kocha huyo wa Manchester United amemwelezea Januzaj kuwa ni mchezaji mzuri na ni vigumu kumzuia anapokuwa na mpira.
"Nakumbuka nilipompa nafasi Rooney katika mechi yake ya kwanza. Januzaj naye ameonyesha uwezo kama aliokuwa nao Rooney. Anafunga mabao na ana uwezo wa kumiliki mpira,"alisema Moyes, ambaye amerithi mikoba ya kocha wa zamani wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson.
"Ni mchezaji aliye kwenye kiwango cha juu na atakuwa mchezaji mwenye kipaji cha aina yake. Ningeweza kumchezesha wiki kadhaa zilizopita, lakini alikuwa majeruhi na sikutaka kufanya kosa hilo,"alisema Moyes.
Kwa upande wake, Rio Ferdinand alisema: "Sitaki kumzunguzia sana, lakini ni mchezaji mwenye kipaji, anaweza kuwa mchezaji wa kiwango cha juu. Atakuwa hazina kubwa ya Manchester United siku zijazo."
Katika hatua nyingine, Chama cha Soka cha England kimewasiliana na klabu ya Manchester United kwa ajili ya kumshawishi Januzaj aichezee timu ya taifa ya England.
Januzaj, ambaye alijiunga na Manchester United 2011, akiwa na umri wa miaka 16, akitokea klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji, bado hajaamua timu ipi ya taifa atakayoichezea. Chipukizi huyo alizaliwa Ubelgiji na wazazi wake wana asili ya Kosovo na Albania.
"Nafikiri kuna njia inayoweza kumfanya awe na sifa ya kuichezea England,"alithibitisha Moyes. "Nafikiri ni suala la uraia."
Januzaj ameishi England kwa miaka mitano na amekuwa akiitwa mara kadhaa kwenye timu ya taifa ya vijana ya Ubelgiji, lakini hajawahi kuichezea. Pia amekuwa akiitwa kwenye timu za taifa za vijana za Albania na Croatia, lakini amekuwa akizitolea nje.
Alipoulizwa iwapo tayari Chama cha Soka cha England kimeshawasiliana na Manchester United kuhusu suala hilo, Moyes alisema: "Ndiyo, wamefanya hivyo."
Mwanasoka mkongwe wa England,Gary Lineker, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa masuala ya soka katika kituo cha televisheni cha BBC alisema, Januzaj ataruhusiwa kisheria kuichezea England kuanzia 2018.
Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), zilizoanza kutumika Mei 2008, kama mchezaji ameishi katika nchi kwa miaka mitano mfululizo baada ya kutimiza miaka 18, anaruhusiwa kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo.
"Hakuna wasiwasi kwamba ni mchezaji mwenye kipaji na macho yetu sote yako kwake, lakini yapo mambo mengi yanayopaswa kujadiliwa kwanza,"alisema Gary.
Kocha Mkuu wa England, Roy Hodson naye amethibitisha kuwa, amekuwa akimtupia macho kinda huyo na anaweza kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo katika siku zijazo.
"Kama atapata uraia, hilo halina shaka,"alisema kocha huyo." Amekuwepo Manchester United kwa kipindi kirefu na bila shaka majadiliano juu ya suala hilo yanapaswa kupewa uzito wakati tutakapoanza kuwapa uraia wachezaji."
Hivi karibuni, Januzaj alikaririwa akisema kuwa, anataka kuichezea Albania, lakini kutokana na uraia wa wazazi wake, anaweza pia kuzichezea Serbia na Uturuki.
Januzaj alianza kuchezea kikosi cha Manchester United katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani dhidi ya Wigan kabla ya kucheza mechi zingine mbili akitokea benchi. Manchester United inataka kumuongezea mkataba wa miaka mitano.
Chipukizi huyo alizaliwa mjini Brussels, Ubelgiji 1995. Alijiunga na Anderlecht akiwa na umri wa miaka 10. Alijiunga na Manchester United, Machi 2011 kwa ada ya uhamisho wa pauni 297,000.
Comments