Na Victor Melkizedeck Abuso
Maelfu ya walimu wamekabiliana na polisi nchini Brazil katika jiji la
Rio de Janeiro na Sao Paulo, wakati wa maandamano ya walimu wakitaka
serikali iwaongezee mshahara.
Walimu wakiandamana nchini Brazil
Makabililano hayo yamezuka baada ya walimu wanaokisiwa kuwa zaidi ya
10,000 kuanza kufanya uharibifu katika majengo ya serikali baada ya
maandamano hayo kuanza kwa amani katika barabara za miji hiyo.
Usiku kucha walimu na polisi wamekimbizana katika mitaa ya jijini la Rio
huku kukiwa na hali ya wasiwasi kipindi hiki suala la usalama likisalia
changamoto kubwa kwa serikali wakati huu nchi hiyo ikijiandaa kuandaa
michuano ya soka ya kombe la dunia mwaka ujao na ile ya Olimpiki mwaka
2016.
Walimu nchini Brazil wamekuwa wakidai nyongeza ya mshahara kwa kipindi
cha miezi mwili sasa, miezi minane kabla ya kuanza kwa michuano ya kombe
la dunia mwaka ujao.
Serikali nchini Brazil inasema imejaribu kushughulikia maswala ya
wafanyikazi wa umma nchini humo hasa katika sekta ya elimu na afya
ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kwa kipindi kirefu.
Maandamano ya Jumatatu usiku ndio makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa
katika nchi hiyo katika siku za hivi karibuni ambayo yalianza kwa njia
ya amani kabla ya kuzuka fujo.
Wanaharakati nchini Brazil wamekosoa sera za rais Dilma Rousseff kuhusu
kutumia fedha nyingi kushughulikia maandalizi ya kombe la dunia na
Olimpiki nchini humo badala ya kushughulikia changamoto za watumishi wa
umma.
Comments