Rais wa Mali Keita avunjilia mbali Kamati ya Mabadiliko ya Jeshi iliyokuwa inaongozwa na Kepteni Sanogo
Na Nurdin Selemani Ramadhani
Rais Mpya wa Mali Ibrahim Boubacar Keita maarufu kwa jina la IBK
amevunjilia mbali Kamati maalum ya Mabadiliko ya Jeshi nchini humo
akisema amechukua uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Rais wa Mpya wa Mali Ibrahim Boubacar KeĂŻta amevunjia mbali Kamati ya Mabadiliko ya Jeshi
REUTERS/Joe Penney
Kamati hiyo iliyokuwa inaongozwa na Kiongozi wa Mapinduzi Kapteni Amadou
Haya Sanogo pamoja na wanajeshi wengi walioshiriki kuiangusha Serikali
ya Rais Amadou Toumani Toure kitu kilichochangia kuibuka kwa machafuko
katika nchi hiyo.
Rais Keita amesema hawezi kuvumilia pale ambapo kuna watu watovu wa
nidhamu hivyo ameona bora avunje mbali kamati hiyo kwa sababu imeshindwa
kufanyakazi yake kama ilivyopaswa.
Kiongozi huyo wa Mali amesema uchunguzi unafanyika kubaini kwa nini
Kamati hiyoimeshindwa kufanyakazi yake ipasavyo na yoyote ambaye
atapatikana na hatia ya kutenda kosa atakabiliwa na adhabu.
Keita amesema hatua ya wanajeshi kufanya mgomo mapema juma hili ni kitu
ambacho hakiwezi kuvumiliwa hata kidogo na kinaonekana kuchochewa na
kamati iliyopewa jukumu la kuhakikisha kuna mabadiliko jeshini.
Rais Keita ambaye amejiapiza kufanya kila linalowezekana katika
kuhakikisha anajenga Jeshi imara litakalokuwa nakibarua cha kuimarisha
hali ya usalama amesema hatoweza kukaa kimya pale atakapoona juhudi zake
zinasitishwa.
Comments