Siku chache baada ya Mkuu wa Wilaya ya
Kisarawe Mkoani Pwani, Mh. Jokate Mwegelo kufanya oparesheni ya kukamata
mifugo katika maeneo ya hifadhi zilizopo wilayani humo, Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina amepiga marufuku tabia ya ukamataji mifugo
kiholela.
Mpina
ametoa marufuku hiyo wakati akifunga maonesho ya 25 ya Nane nane Kanda
ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na
Morogoro katika viwanja vya Mwalimu JK Nyerere mjini Morogoro.
Mpina amesema katika siku za hivi
karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuendesha
operesheni za kukamata mifugo na kuifungia bila kuipatia huduma muhimu
ikiwemo maji, malisho na matibabu na matokeo yake mifugo mingi hufa na
kusisitiza kuwa operesheni hizo zinapofanyika ni lazima zihusishe pia
maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwa na uelewa wa pamoja wa
jambo hilo.
Aidha Mpina alisema utaratibu
unaofanyika hivi sasa wa kukamata hovyo mifugo ni ukiukwaji wa sheria
namba 17 ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003 na, Sheria ya Ustawi wa
Wanyama Namba 19 ya Mwaka 2008 ambazo zinataka mifugo inapokamatwa
kuzingatia masuala ya magonjwa na ustawi wa mifugo katika kipindi chote
inapokuwa imeshikiliwa.
Katika hatua nyingine, Mpina pia
alielezea kutoridhishwa na utoaji wa mikopo wa Benki ya Kilimo (TADB)
ambapo kwa taarifa iliyotolewa sekta ya uvuvi hakuna mkopo wowote
uliotolewa katika mwaka wa fedha uliopita huku upande wa sekta ya mifugo
wakiambulia wajasiamali wanne tu .
Aidha kiasi cha jumla ya mikopo
iliyotolewa ya Sh. Bilioni 39 kwa mwaka mzima ni kidogo sana
ikilinganishwa na mahitaji wa mikopo katika sekta za kilimo,mifugo na
uvuvi, huku akipongeza kazi nzuri inayofanywa na Taasisi ya PASS na
SAGGOT-CTF katika kuwadhamini wakulima , wafugaji na wavuvi katika
kupata mikopo.
Kutokana na changamoto hizo, Waziri
Mpina ameitaka benki hiyo kurekebisha kasoro zilizopo na kujipanga
vizuri kuhudumia sekta hizo, vile vile amewaagiza makatibu wakuu wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuitambua na kupitia miradi yote ya
wajasiriamali katika sekta zao ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa
wakati.
Sambamba na hilo amewaagiza wakurugenzi
wa halmashauri zote nchini kupitia idara ya maendeleo ya jamii na idara
ya ushirika kuwaandaa na kuwaunganisha wananchi katika kukidhi vigezo
vya kupata mikopo katika taasisi za fedha.
Pia aliagiza Halmashauri zote nchini
kuwatambua vijana wanaohitimu mafunzo katika vyuo vya ugani vya SUA,
FETA, LITA na ATI na kuwatumia katika safari ya kuleta mageuzi ya
uvuvi,mifugo na kilimo katika maeneo yao na kwamba hata mikopo ya
asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake,vijana na walemavu kundi hili la
wagani liangaliwe kwa jicho la pekee.
Mbali na hilo Waziri Mpina alisema
pamoja na Serikali kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi wa mialo na
masoko ya samaki baadhi ya halmashauri zimetelekeza miundombinu hiyo na
kuendelea kutoa huduma katika maeneo yasiyo rasmi, pia baadhi ya mialo
na masoko haifanyiwi matengenezo wala ukarabati kiasi cha kukosa huduma
muhimu kama maji, vyoo, umeme na majokofu ya kuhifadhia samaki hali
inayosababisha usumbufu na hasara kwa wananchi licha ya kutozwa ushuru
kila uchao.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mpina ametoa
miezi mitano kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinakarabati na
kuweka huduma muhimu na kwamba wataoshindwa kufanya hivyo mialo na
masoko hayo yatarejeshwa chini ya usimamizi wa Wizara na halmashauri
hizo hazitaruhusiwa tena kukusanya mapato yatokanayo na sekta hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa
Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alimhakikishia Waziri Mpina kuwa
maagizo yote aliyotoa watayafuatilia na kuyasimamia ili kuona
utekelezaji wake kwani Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuleta
mageuzi ya kweli katika sekta za Kilimo,Mifugo na Uvuvi.
Pia Ndikilo alisema ni jambo la
kusikitisha kuona licha ya fursa kubwa za mifugo na uvuvi zilizoko
katika mikoa ya Kanda ya Pwani lakini hadi sasa hakuna kiwanda hata
kimoja cha kuchakata samaki wala nyama na kumuomba Waziri Mpina kuandaa
kongamano ya mikoa hiyo ili kujadili kwa pamoja namna ya kuwekeza katika
viwanda vya kuchakata bidhaa hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe
Stephen Kebwe alisema maonesho hayo ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio
makubwa kwani wakulima,wafugaji na wavuvi na makundi mengine
yamejitokeza kwa wingi na wamepata fursa ya kujifunza teknolojia mpya
zitakazoboresha uzalishaji.
Maonesho hayo yalihudhuriwa na wakuu wa mikoa, wilaya, mameya, wakurugenzi wa halmashauri,madiwani pamoja na sekta binafsi.
Comments