Na Mwandishi Wetu
Aliyekuwa mmiliki wa IPTL Harbinder Singh Sethi ameieleza Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ana miezi 6 hajaonana na mke wake.
Sethi ambaye yupo katika gereza la Ukonga ameyaeleza hayo mbele ya
Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi baada ya Wakili wa serikali Mwanaamina
Kombakono kueleza kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya Wakili Kombakono kueleza hayo, Wakili wa Sethi, Dorah
Mallaba aliieleza mahakama kuwa bado hawajapata kibali kwa ajili ya
mshtakiwa Sethi kuonana na mkewe. Hata hivyo Wakili Mallaba aliiomba
mahakama iruhusu hata kwa dakika 5 Sethi aonane na mkewe.
“Naomba mahakama itumie busara kwa kuwa mke wake yupo hapa mahakamani, aweze kuonana naye hata kwa dakika 5,”ameomba.
Wakili Kombakono baada ya kusikiliza hoja ya wakili Mallaba, alieleza kuwa kuna taratibu za kumuona mahabusu hivyo zifuatwe.
Kutokana na maombi hayo Hakimu Shahidi amesema taratibu za kuwatunza
mahabusu zipo chini ya Magareza kama kuna jambo lolote mahususi basi
lifikishwe mahakani, ambapo ameahirisha kesi hiyo hadi September
13,2018.
Katika kesi hiyo Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya
uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu ,
kighushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za
udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha hasara ya USD 22,
198,544.60 na Sh 309,461,300,158.
Comments