Wakazi wa Mkoa wa Singida
wanaoendeleza mila potofu ya ukeketaji, wameaswa kuachana na mila hiyo,
badala yake waanzishe vilabu kwa lengo la kuwafundisha wasichana umuhimu
wa kufanya kazi halali na maadili mema kupunguza kasi ya mmomonyoko wa
maadili.
Mwito huo ulitolewa na Dk Getrude Mughamba kutoka Halmashauri ya Wilaya
ya Singida wakati wa warsha iliyohudhuriwa na vikundi kazi na watendaji
wa kata, wanaoshiriki utekelezaji wa mradi wa kutokomeza vitendo vya
ukeketaji.
Mradi huo unaotekelezwa katika kata nne za halmashauri hiyo, unaendeshwa
na Shirika la Empower Society to Transform Lives (ESTL) kwa ufadhili wa
Shirika la Foundation for Civil Society. Dk Mughamba alieleza kuwa
kupitia vilabu hivyo, wasichana watapata fursa ya kufundishwa mapishi
bora, usafi na utunzaji wa mazingira na namna bora ya kuishi na mume;
hivyo kurejesha nidhamu na maadili mema ya namna ya kuishi katika jamii
iliyostaarabika.
Alisema kuwa jamii ya kabila la Wanyaturu na makabila mengine
yanayoendelea kukumbatia mila hiyo potofu ya ukeketaji ambao wamekuwa
wakifanya hivyo kwa ajili ya kujipatia sifa ya kuolewa hivi sasa hawana
budi kubadili mfumo wa mila na utamaduni wenye tija. Alisema kuwa kwa
kuanzisha vilabu vya aina hiyo, jamii itawafunda watoto wao kwa namna
bora zaidi, badala ya kuendelea kuwakeketa hali inayowatia kwenye
machungu ya kujifungua kwa taabu, kutofurahia vyema tendo la ndoa na
kuwaathiri milele kisaikolojia.
Comments