Serikali imesema
kufikia mwaka 2020 malengo yake ni kuhakikisha asilimia 45 ya wanawake
walioolewa wanatumia huduma za uzazi wa mpango huku ikibainisha kwa sasa
asilimia 32 wanatumia huduma hizo lengo likiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto
vitokanavyo na uzazi.
Hayo yamesemwa
leo jijini Dar es Salaam na Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu wakati akiwa na Ujumbe wa Waziri wa Maendeleo wa Uingereza,
Penny Mordaunt auliotembelea katika Zahanati ya Tabata ‘A’ wilayani Ilala ili
kuangalia huduma za uzazi wa mpango zinavyotolewa zahanati hapo.
Amesema
Serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikia na Serikali ya Uingereza imekuwa
mstari mbele katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kupitia huduma
hizo na kwamba lengo ni kupunguza vifo hivyo.
“ Waziri Penny amekuja kuangalia changamoto ya
afya mama na mtoto na fedha wanazotoa tunazifanyia kazi inayokusudiwa kwani Serikali yetu na ya
Uingereza zinashirikiana katika kuboresha huduma ya mama na mtoto,” amesema.
Amebainisha
kuwa takwimu zinaonyesha wanawake 556,000 wanafariki kutokana na vifo vifo vya
uzazi katika kila vizazi hai 100,000.
Amesisitiza
kuwa uzazi wa mpango unaweza kupunguza vitokananvyo na uzazi kwa asilimia 30 na
kubainisha Serikali inaendelea kutenga rasilimali fedha za ndani kuboresha
huduma za afya ikiwemo kuajiri watoa huduma za afya.
Kwa upande
Waziri Penny amesema kuwa amefurahishwa alivyojionea huduma za uzazi wa mpango
zinavyotolewa kwenye zahanati hiyo na kumpongeza Waziri Ummy kwa umahiri wa
kusimamia utolewaji wa huduma hizo nchini hapa.
Akiwa katika
Zahanati hiyo waziri huyo na ujumbe wake ametembelea Jengo la Kliniki ya Baba,
Mama na Mtoto pamoja na Kikundi cha Umoja Group kinachojihusisha na Uzazi wa
Mpango.
Naye Mganga
Mkuu Mfawidhi wa Zahanati ya Tabata ‘A’, Modest Mwinuka amesema zahanati Hiyo
ni miongoni mwa vituo 88 vinavyotoa huduma ya afya ya mama na mtoto katika
manispaa ya Ilala huku akisisitiza kati ya vituo hivyo, vituo 51 vinatoa huduma
ya uzazi wa mpango.
Amesema
zahanati hiyo inahudumia wakazi kutoka mitaa nane ikiwemo Tabata, Msimbazi,
Tenge, Mandela, Mtambani, Msimbazi Magharibi,Matumbi pamoja na Tabata Kisiwani
yenye wakazi74,742 kati yao wananume ni 18,593, wananwake 38,833 walio kwenye
umri wa kuzaa ni 13,454.
“ Zahanati
ina watumishi wapatao 29 wa kada mbalimbali wakiwemo waganga na wauguzi, kati
yao 28 wamepatiwa mafunzo ya uzazi wa mpango, huduma rafiki kwa vijana, huduma
baada ya mimba kuharibika na ukatili wa kijinsia,” amesema Mwinuka.
Mganga huyo
ameongeza kuwa njia za huduma ya uzazi wa mpango zinazotolewa katika zahanati
hiyo ni njia za muda mfupi ambazo ni vidonge, sindano, kondomu za kike na za
kiume pamoja na njia ya shanga, njia ya muda mrefu(Kitanzi na vijiti), pamoja
na nyingine za kudumu(kufunga kizazi mwanamke/mwanaume).
Comments