Na Mwandishi Wetu, GENK
NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amefunga bao la pili la timu yake, KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Lech Poznan ya Polandkatika mchezo wa kwanza, Raundi ya Tatu ya mchujo UEFA Europa League Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
Samatta alifunga bao hilo dakika ya 56, baada ya kiungo wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy kutangulia kufunga la kwanza dakika ya 44.
Sasa Genk watahitaji kwenda kuulinda ushindi wao katika mchezo wa marudiano Agosti 16, Uwanja wa INEA mjini Poznan ili kwenda katika mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi, ambako watacheza mechi moja zaidi nyumbani na ugenini.
Mbwana Samatta akishangilia baada ya kuifungia Genk jana katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Lech Poznan ya Poland
Samatta aliyejiunga na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya DRC, ambayo nayo ilimtoa Simba SC ya nyumbani, Tanzania mwaka 2011 anawindwa na klabu kadhaa za Borussia Dortmund ya Ujerumani, Levante ya Hispania na CSKA Moscow ya Urusi.
Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa: Vukovic, Lucumi, Dewaest, Maehle, Berge, Malinovskyi, Pozuelo, Trossard/Zhegrova dk81, Ndongala na Samatta/Gano dk63.
Lech Poznan : Buric, De Marco, Rogne/Vujadinovic dk67, Tralka, Gajos, Jevtic/Tomczyk dk73, Makuszewski/Jozwiak dk53, Cywka, Kostevych, Orlowski na Gytkjaer.
Comments