Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa 41 wa umoja wa kikanda wa makampuni ya bima ya nchi za Mashariki na kusini mwa Afrika (OESAI) ukiwa na lengo la kuendeleza vipaumbele vya kukuza soko la bima.
Katika mkutano huo Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mipango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 41 wa Umoja wa Kikanda na Makampuni ya Bima ya Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika(OESAI) unaotarajiwa kufanyika kwenye Hoteli ya Mount Meru kuanzia Agosti 27 hadi 29 mwaka huu.
Pichani kamishna wa bima wa mamlaka ya usimamizi wa shughuli za bima nchini (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware wakati akitoa taarifa ya mkutano huo mbele ya waandishi wa habari hawapo pichani leo.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Mamlaka ya usimamizi wa shughuli za bima nchini (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware wakati akitoa ufafanuzi kwa wanahabari kuhusiana na mkutano huo.
Amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) kwa kushirikiana na umoja huo wameamua kuufanaya hapa nchini na kwamba lengo lake ni kujadili usimamizi bora wa makampuni ya bima, kuangalia namna bora ya huduma za bima ziwafikiea wateja kwa kutumia teknolojia ya teknohama.
“ Tunategemea makampuni na taasisi za bima zitakazoshiriki zitabadilishana uzoefu na kufungua fursa za masoko achilia mbali hilo zitaunaganisha uzoefu kwenye bima za kilimo na ufugaji,” amesema.
Amebainisha kuwa mkutano utashirikisha nchi 33 wanachama na kwamba wageni zaidi ya 300 wanatarajiwa kuingia mjini huo huku akisisitiza utafungua fursa nyingi za kibiashara kwa wenyeji wa mji huo.
Kwa upande wake Mjumbe wa mkutano wa umoja huo, Margaret Ikongo amesema taasisi hiyo imeanzishwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu kwa wananchama na kwamba hii mara pili Tanzania kupewa heshima ya kufanyika.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo, Khamis Suleiman amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwa kuwa unakutanisha nchi tofauti huku akibainisha lengo ni kuvuka asilimia 15 ya watanzania wanaotumia bima.
Amefafanua kuwa washiriki ambao hawana uzoefu wa masuala ya bima ya kilimo na mifugo watajifunza kutoka kwa makampuni mengine ikiwemo matumizi ya teknohama kuongeza watumiaji wa huduma za bima.
Comments