Uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Taifa ya Jeshi la Polisi la Kenya (NPSC)
umeongeza matarajio ya jeshi la polisi lililoandaliwa vizuri linaloweza
kushughulikia changamoto za sasa za ulinzi na uwezekano wa vitisho
wakati wa uchaguzi wa Machi 2013.
Ofisa wa polisi wa Kenya akilinda doria mitaa ya Mombasa. Baada ya
wajumbe wa Tume ya Taifa ya Jeshi la Polisi kuthibitishwa, polisi
watakuwa chini ya mamlaka moja. [Simon Maina/AFP]
Kaimu Katibu wa Baraza la Mawaziri Francis Kimemia aliwatangaza
waliyoteuliwa tarehe 6 Septemba na majina yaliwasilishwa kwa bunge siku
iliyofuata. Bunge limepewa hadi tarehe 28 Septemba kupitia waliyoteuliwa
na kuomba majina mapya kama kutakuwa na wowote watakaokataliwa.
Mchakato wa kuanzisha NPSC ulikuwa umecheleweshwa tangu Agosti 2011 kwa
sababu ya kutokubaliana kati ya Waziri Mkuu Raila Odinga na Rais Mwai
Kibaki kuhusu waliyoteuliwa.
Waliyopendekezwa katika tume ni Johnstone Kavuludi kama mwenyekiti, na
Ronald Musengi, Esther Chui-Colombini, Murshid Mohamed, Major Muiu Mutia
na Mary Owuor kama wajumbe.
NPSC itakuwa na madaraka ya kuchunguza, kuajiri, kufukuza, kuadhibu na
kuwahamisha maofisa wa polisi. Tume pia itasaidia kutekeleza masharti
mapya ya katiba ya kuweka chini ya makao makuu uongozi wa vitengo
mbalimbali vya polisi, ambavyo awali vilifanya kazi kwa kujitegemea.
"Kuundwa kwa tume ni hatua kubwa ambayo itasaidia kurekebisha jeshi letu
la polisi na kutoa muundo muhimu wa kupambana na hali ya kutokuwa na
usalama na kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki," alisema Fred Kapondi,
mwenyekiti wa kamati ya idara ya bunge ya Utawala na Usalama wa Taifa.
Comments