Dk Mary Nagu |
MBIO za uchaguzi
ndani ya CCM zimefikia patamu, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu kuenguliwa kugombea nafasi
ya Ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hanang’, huku Mke wa Rais, Salma
Kikwete akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo Lindi Mjini.
Habari kutoka Hanang’ zimeeleza
kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo imemwengua Dk Nagu na
kuwabakiza wagombe wawili, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na
Leonsi Marmo.
Taarifa kutoka kwenye kikao
hicho kilichofanyika juzi katika Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo na
kuhudhuriwa na wajumbe 12 zimeeleza kuwa Dk Nagu ameenguliwa kutokana
na maelezo kuwa kanuni hazimruhusu kugombea.
Chanzo cha habari kimeeleza
kuwa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu kwenye kinyang’anyiro hicho ni ile
inayowataka viongozi wenye kazi za kila siku; ubunge na uwaziri
kutogombea.
Katika hatua nyingine Mke wa Rais, Salma Kikwete amerudisha fomu ya kuwania ujumbe wa Nec Taifa kupitia Wilaya ya Lindi Mjini.
Katibu wa CCM Wilaya ya Lindi
Mjini Mohamed Kateva, alisema jana kwamba Salma ni mgombea pekee
aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo katika wilaya yake.Kateva alisema
mwisho wa kurudisha fomu ilikuwa Agosti 28, mwaka huu na mpaka tarehe
hiyo hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwa amejitokeza kuwania nafasi hiyo.
Habari hii kwa hisani ya Hakingowi
Comments