Mali imeuomba Umoja wa Mataifa
utoe kibali cha haraka kwa jeshi la kimataifa liisaidie serikali ya
nchi hiyo izidhibiti tena sehemu za kaskazini ya nchi hiyo.
Habari hiyo imetolewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius.
Nchi hiyo ya Afrika magharibi ilitumbukia katika michafuko mwezi Machi
mwaka huu, pale wanajeshi walipompindua kutoka madarakani rais, hivyo
kuweko pengo wazi la madaraka. Hali hiyo iliwawezesha waasi wa
Ki-Tuareg kutwaa thuluthi mbili ya nchi hiyo. Lakini makundi ya
kiislamu, baadhi yao yakiwa na ushirikiano na mtandao wa Al-Qaeda,
yaliuteka nyara uasi huo katika sehemu za kaskazini ya nchi na
kuanzisha kutekelezwa sheria za kiislamu.
Akiiashiria barua iliopelekwa na viongozi wa mpito wa Mali kwa katibu
mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, hapo Septemba 18, Laurent Fabius
alisema Mali imeomba lipitishwe azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa chini ya Ibara ya Saba ya Hati ya Umoja huo ili kutolewe kibali
cha kutumiwa jeshi la kimataifa lilisaidie jeshi la Mali kuyateka tena
maeneo ya kaskazini mwa Mali. Ibara hiyo ya Saba inaliruhusu baraza la
usalama litoe kibali cha kuchukuliwa hatua kutoka zile za kibalozi na
za kiuchumi hadi kujiingiza kijeshi.
Laurent Fabius, akiisoma barua hiyo, aliwaambia waandishi wa habari
kwamba kwa miezi kadha Mali imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa usalama
usiowahi kuonekana kabla katika maeneo yake ya kaskazini ambayo
yametawaliwa na makundi yenye silaha, wakiwemo magaidi, wasafirishaji
wa mihadharati na aina zote za wahalifu. Alisema serikali ya Mali
inataka jeshi la aina hiyo lipelekwe kwa haraka ili kuyasaidia majeshi
ya usalama ya Mali kutekeleza shughuli hiyo.
Comments