Na Mohammed Mhina, Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imeainisha mpango wa matumizi ya fedha shilingi Bilioni 14.8
zilizotolewa kama msaada na Serikali ya China kwa SMZ.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake leo mjini Zanzibar, Waziri wa Fedha wa SMZ Mh.
Omar Yusuf Mzee, amesema kuwa
kipaumbele cha kwanza katika fedha hizo itakuwa ni kuboresha huduma za
Afya, Elimu na miundombinu ya maji pamoja na uwekaji wa taa za sola
kwenye baadhi ya barabara za mji wa Zanzibar.
Akizungumzia huduma za Afya,
Waziri huyo wa fedha amesema kuwa sehemu ya fedha hizo zitasaidia
upanuzi na ujenzi wa Hospitali ya Mkoani Kisiwani Pemba na kuifanya kuwa
ya rufaa.
Waziri Mzee amesema taratibu
zote za ujenzi wa Hospitali hiyo imekamilika na kwamba mara ujenzi huo
utakapokamilika hakutakuwa na haja tena ya wagonjwa mahututi kuletwa
katika Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja kwa vile Hospitali hiyo itakuwa na
kila aina ya vifaa na madawa ya tiba.
Amesema fedha hizo pia
zitasaidia kuwasomesha wataalamu wa afya, Walimu wa masomo ya sayansi na
kuboresha shule ya msingi ya Mwanakwerekwe kwa kuongeza ujenzi wa
vyumba 12 vya madarasa.
Mh. Mzee amesema kuwa sambamba
na hayo, fedha hizo pia zitasaidia kuweka taa za sola katika kwenye
baadhi ya barabara za mji wa Zanzibar na kuboresha miundombinu ya maji
mijini na Vijijini.
Comments