Afisa
wa ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya
amani,Herve Ladsous amesema waasi wa M23 mashariki ya jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo wameanzisha serikali yao na kutoza watu ushuru.
Mkuu huyo wa Umoja wa mataifa
anayehusika na masuala ya usalama anasema waasi wa kundi la M23
wamejiundia serikali yao wenyewe mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo.
Baada ya kukutana na wanachama
wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa nchi hiyo,
Ladsous amewaambia waandishi wa habari kwamba kuna hali ya utulivu kiasi
tangu wiki kama tano au sita zilizopita lakini hapana shaka hilo
linaweza kubadilika haraka sana kuelekea pande zote.
Akizungumzia kitendo cha waasi
kujitangazia serikali yao na kukusanya ushuru Naibu Gavana wa Jimbo la
Kivu ya Kaskazini, Lutahichwa Mulwa Ale amesema ni jukumu la serikali
kukomesha kitendo hicho na kuwasaidia wananchi wa mkoa wa Kivu ya
Kaskazini.
Kundi la M23 likiongozwa na
Bosco Ntaganda anayetakiwa na mahakama ya Kimataifa inayoshughulikia
kesi za Uhalifu limeudhibiti mkoa wa Kivu ya Kaskazini karibu na mpaka
wa nchi za Rwanda na Uganda.Wataalamu wa Umoja wa Mataifa pamoja na
serikali ya Kongo wanaituhumu Rwanda kwamba inawaunga mkono waasi hao
walioanzisha harakati zake za hujuma mwezi Aprili.
Comments