MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya Tanzania Bara, Simba leo wanaendelea na kampeni za kuwania tena taji hilo kwa kumenyana na Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo linatarajiwa kuanza saa 11 jioni na litaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini.
SuperSport imeingia mkataba na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) wa kuonyesha moja kwa moja mechi tano za ligi hiyo zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa na Chamazi, Dar es Salaam.
Kituo hicho kilianza kazi hiyo jana kwa kuonyesha moja kwa moja mechi kati ya Azam na JKT Ruvu iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa. Katika mechi hiyo, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho wakati Yanga itakapomenyana na African Lyon kwenye uwanja huo huo. Pambano hilo pia limepangwa kuanza saa 11 jioni.
Oktoba Mosi mwaka huu, Mtibwa Sugar itashuka dimbani kwenye uwanja wa Chamazi kumenyana na Ruvu Shooting kuanza saa 10.30 jioni.
Mahasibu wa soka nchini, Simba na Yanga watashuka dimbani Oktoba 3 mwaka huu, katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa litakalofanyika kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa moja usiku.
Comments