Jeshi la Umoja wa Afrika nchini
Somalia (AMISOM) pamoja na Jeshi la Kenya wamethibitisha kupambana na
wanamgambo wa al-Shabaab ndani ya mji wa bandari wa Kismayo, wakidai
kukaribia kuuchukua mji huo muhimu kimkakati.
"Lengo la AMISOM ni kuwakomboa watu wa Kismayo na kuwawezesha kuendelea
na maisha yao kwa amani, utulivu na usalama. Operesheni zetu
zinaendelea kulenga shabaha maalum za al-Shabaab mjini Kismayo,"
alisema Kamanda Andrew Gutti wa AMISOM, akiwataka wapiganaji wote wa
al-Shabaab walio ndani ya Kismayo kuweka chini silaha zao.
Katika hatua nyengine, Jeshi la Kenya limesema kwamba wapiganaji wake
wamelichukua eneo la kusini ya Kismayo, ngome ya mwisho ya kundi la
al-Shabaab.
Msemaji wa Jeshi hilo, Cyrus Oguna, aliliambia shirika la habari mapema
leo kwamba wanajeshi wa Kenya walikumbana na upinzani mdogo wakati wa
kuliteka eneo hilo.
Al-Shabaab, wakaazi wa Kismayo wakanusha
Hata hivyo, wakaazi wa huko pamoja na wanamgambo wa al-Shabaab
wamekanusha taarifa hizo, wakisema kwamba ndio kwanza wanajeshi wa
Kenya walikuwa kwenye viunga vya mbali na Kismayo, ambako wamekuwako
kwa zaidi ya siku nne sasa.
Comments