Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imebariki kuondolewa kwa
majina ya baadhi ya vigogo wakiwamo wabunge kuwania nafasi ndani ya
chama hicho, maamuzi yanayotoa picha ya kung’oa watu wenye tuhuma
mbalimbali.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya kikao hicho, kazi kubwa ambayo
imefanywa na Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho iliungwa mkono
na CC, huku wajumbe wa vikao hivyo viwili wakimpongeza Mwenyekiti wa
chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kwa kuridhia maamuzi magumu.
Kikao cha CC ambacho kilifanyika juzi kuanzia mchana na kumalizika saa
6:30 usiku, kilielekeza shoka lake kwa majina yote ya wabunge waliowania
nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambao walihusika
katika utiaji saini azimio la kumung’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
mapema mwaka huu.
Wabunge hao walisaini katika fomu maalum iliyoandaliwa na Mbunge wa
Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, kwa ajili ya kupiga kura ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
Wabunge hao walichukuliwa uamuzi huo ili kuishinikiza serikali
kuwafukuza mawaziri ambao wizara zao zilitajwa katika ripoti ya Mkaguzi
na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati kwa kashfa
mbalimbali na kuisababishia serikali hasara.
Wabunge wa CCM waliotia saini ni Nimrod Mkono ambaye ni Mbunge wa Musoma
Vijijini, anayewania nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na;
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe ambaye anagombea ujumbe wa NEC
kupitia Wilaya ya Ludewa na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina. Wote
wamekatwa.
Mwingine ambaye jina lake limekatwa ni Mbunge wa Ilala na Mwenyekiti wa
Bunge, Mussa Zungu ambaye ameomba kupendekezwa kugombea uenyekiti wa
Jumuiya ya Wazazi Taifa.
Comments