Mamlaka ya Vitambulisho imevunja mikataba ya wafanyakazi wake 597
kutokana na ufinyu wa bajeti na ufanisi mdogo katika kuzalisha
vitambulisho vya taifa.
Mamlaka hiyo itapitia upya majukumu ya wafanyakazi wengine 802 wa
kudumu ili kuendana na majukumu yaliyopo. Kama itabainika idadi bado ni
kubwa, watarudishwa wizara ya utumishi kwa ajili ya kupangiwa majukumu
mengine.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, Kaimu
Mkurugenzi wa Nida, Dk Modestus Kipilimba alisema mamlaka hiyo imekuwa
na wafanyakazi wengi, lakini kazi iliyokusudiwa ya kutengeneza
vitambulisho vya Taifa haifanyiki kikamilifu.
Dk Kipilimbi alisema wafanyakazi 1,399 waliopo Nida walitakiwa
kuzalisha vitambulisho 24,000 kwa siku, lakini waliweza kuzalisha
vitambulisho 1,200 kwa siku nchi nzima ambayo ni sawa na asilimia tano.
“Kuanzia leo (jana) ninawatangazia watumishi wa mkataba kwamba Nida
hakuna kazi kwa sasa. Tutapitia upya masharti ya mikataba yao na kufuata
utaratibu wa kisheria,” alisema.
Alisema lengo kubwa la Nida ni kuongeza ufanisi katika utendaji ili
kuhakikisha kwamba ifikapo Desemba 31, mwaka huu kila mwananchi awe n
kitambulisho chake.
Alisema kuna namna nyingi za utambulisho wa Taifa ikiwa ni pamoja na
vitambulisho vyenyewe kuhifadhi taarifa kwenye tanzidata na namba za
simu zake.
Mkurugenzi huyo ambaye aliteuliwa Februari 15 kushika wadhifa huo,
alisema lengo lao jingine ni kuinua matumizi ya utambulisho wa Taifa.
Katika kutekeleza hilo, alisema watakutana na wadau mbalimbali ili
kukifanya kitambulisho cha Taifa kihifadhi taarifa mbalimbali za
wananchi.
“Pia, tunafanya uhakiki wa mikataba yote ambayo Nida imeingia ili
kujiridhisha kama sheria ya manunuzi ilifuatwa. Kama kuna mikataba
ambayo haikufuata taratibu, basi tutaangalia utaratibu wa kisheria,”
alisema.
Alisema Nida inatarajia kupokea mashine za BVR 5,000 kutoka Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili kutumia kutengeneza vitambulisho vya Taifa
ambavyo vitakuwa na saini ya mwenye kitambulisho hicho na anayekitoa.
“Tumepokea maoni ya watu wengi wakionyesha umuhimu wa saini kwenye
kitambulisho, kama Rais (John) Magufuli alivyosema. Kwa hiyo,
tunakamilisha taratibu za kubadilisha kanuni ili vitambulisho
tutakavyoendelea kuvitoa viwe na saini,” alisema.
Hata hivyo alisistiza kwamba vitambulisho ambavyo havina saini
vitaendelea kutumika na kutambuliwa kwa sababu saini ipo kwenye nyaraka
nyingine.
Alisema Nida itaruhusu pia wananchi kwenda kubadilisha na kupata vitambulisho vyenye saini.
Lengo la mabadilikp haya ni kuongeza ufanisi kwa uwajibikaji. Hasara
iliyopatikana ni kubwa sana, hatutaki tuendelee kubeba msalaba huu
wakati lengo kuu halijatimia,” alisema Dk Kipilimba.
Chanzo: Mwananchi
Comments