Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku nane kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Busega, Hamis Yuna, kuhamia kwenye halmashauri hiyo
kutokana na kuishi nyumba ya kulala wageni iliyopo wilaya jirani ya
Magu.
Pia, Majaliwa ametoa siku 13 kwa watumishi wote wanaoishi Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, kuhamia wilaya hapa ifikapo Machi 15.
Akihutubia wakazi wa Kata ya Lamadi wilayani hapa jana, Majaliwa
alisema hatapenda kumuona mtumishi kufanya kazi akitokea wilaya nyingine
ilhali kuna nyumba nyingi za kutosha.
Alisema watumishi wanaoshindwa kuishi maeneo yao ya kazi, wanawakosesha huduma wananchi wanaotegemea.
Majaliwa alisema haiwezekani mtumishi kuishi wilaya nyingine na
kufanya kazi kwingine na kwamba, muda mwingine hufunga mapema ofisi ili
kuwahi usafiri.
“Nampa siku nane mkurugenzi kuhamia makao makuu ya wilaya hiyo na
watumishi wote kufikia tarehe 15 wawe wamehamia hapa, mkuu wa wilaya
utanijulisha kama wameshahamia ili tuje tuone aliyekataa kuhamia makao
makuu ya wilaya tujue hatua za kuchukua,” alisema Majaliwa.
Tangu kuundwa kwa wilaya hiyo watumishi wengi wamekuwa wakiishi Wilaya ya Magu, kwa madai kuwa hakuna nyumba za kutosha.
“Nimetembelea na kuona makao makuu ya wilaya hii, kuna nyumba nyingi
kiasi kwamba hakuna mtumishi ambaye ataweza kukosa kuishi, tukihamia
hapa tutawahudumia wananchi vizuri tofauti na sasa tunafanya kazi ili
kuwahi kuondoka,” alisema Majaliwa.
Majaliwa yupo kwenye ziara ya kwanza tangu Serikali ya Awamu ya Tano
ichaguliwe, imeanzia Mkoa wa Simiyu baadaye anatarajiwa kwenda Mwanza,
Geita na Kagera kukagua shughuli za maendeleo kutatua kero za wananchi.
Chanzo: Mwananchi
Comments