Siku moja baada ya kuugua ghala na kulazwa kwenye chumba cha
uangalizi maalumu (ICU), katika Hospitali ya Hindu Mandal, Dar es
Salaam, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad,
amesema uchovu wa safari ni chanzo cha afya yake kuzorota.
Maalim Seif, ambaye jana aliruhusiwa kutoka hospitali, amesema
alikuwa anasumbuliwa na uchovu wa safari, baada ya kutoka India,
alikokuwa amekwenda kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo jana, Maalimu
Seif alisema hali yake iko imara, baada ya kupatiwa vipimo hospitalini
hapo.
“Niko fiti kama mnavyoniona, Ninaweza kutembea kutoka hapa hadi Kibaha,” alisema Maalim Seif.
Alisema wiki iliyopita alikuwa nchini India kwa ajili ya matibabu na alirejea nchini Ijumaa na kwenda moja kwa moja Zanzibar.
“Jana (juzi) wakati nikija jijini hapa kwa ajili ya ratiba zangu za
vikao kwa jioni, nilianza kujisikia kizunguzungu tangu nikiwa airport
(uwanja wa ndege). Nililazimika kupanda ndege hivyo hivyo, nilipofika
Dar es Salaam, nililetwa moja kwa moja hadi hapa hospitalini,” alisema
Maalim Seif.
Alisema kwa sasa anaendelea vizuri na kwamba alikuwa akitarajia kuruhusiwa kwenda nyumbani jana jioni.
“Ninawashukuru wananchi, Wazazibari na Watanzania wote na wale
walioko nje ya nchi wameonyesha mapenzi makubwa kwangu. Kweli wananchi
wana mahaba na mimi, kwani wapo waliosikia nimelazwa na kuanza kuzimia,
naomba niwajulishe ninaendelea vizuri na leo nitaruhusiwa,” alisema.
Kwa upande wake, Daktari wa Maalim Seif, Omary Suleiman, alisema
walikwenda India na kwamba Maalim Seif alifanyiwa upasuaji wa uti wa
mgongo na kurejea salama nchini.
“Tulirudi Ijumaa tukaenda Zanzibar na wakati anarudi Dar es Salaam
jana kwa ajili ya shughuli za ratiba ya kikazi jioni alishikwa na
kizunguzungu lakini haikutuzuia kusafiri kwa sababu ya majukumu yake ya
kikazi kwani alikuwa na vikao,” alisema.
Alisema uchunguzi uliofanywa na madaktari hakuna ugonjwa wa aina
yoyote unaomsumbua bali ni uchovu na kwamba hali yake inandelea nzuri.
Chanzo: NIPASHE
Comments