Katibu mkuu mpya wa Chadema atajulikana leo wakati Mwenyekiti wa
chama hicho, Freeman Mbowe atakapowasilisha jina la mtu anayempendekeza
kushika wadhifa huo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalim alisema jana kuwa jina
hilo linatarajiwa kuwasilishwa mbele ya kikao cha Baraza Kuu kinachoanza
hapa leo.
Moshi mweupe kuhusu jina la katibu mkuu mpya utaonekana Jumamosi mchana (leo). Mimi na Naibu Katibu Mkuu mwenzangu John Mnyika tuko tayari kumpokea bosi mpya,” alisema Mwalimu.
Moshi mweupe kuhusu jina la katibu mkuu mpya utaonekana Jumamosi mchana (leo). Mimi na Naibu Katibu Mkuu mwenzangu John Mnyika tuko tayari kumpokea bosi mpya,” alisema Mwalimu.
Katika kikoa chake na waandishi wa habari kilichohudhuriwa na Mnyika,
Kaimu Katibu Mkuu huyo alisema hadi sasa, hakuna yeyote miongoni mwa
viongozi na wanachama wa Chadema anayejua kwa hakika nani atarithi
mikoba hiyo iliyoachwa na Dk Willibrod Slaa zaidi ya Mbowe.
Alipoulizwa jana, Mbowe hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani
zaidi ya kuahidi kumteua katibu mkuu atakayemudu kubeba dhamana ya
kuivusha Chadema salama katika harakati za kushika dola katika uchaguzi
mkuu ujao wa mwaka 2020.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema:
“Tunaweza kufikia uamuzi kwa maridhiano bila hata wajumbe kulazimika
kupiga kura. Hilo naweza kukuhakikishia kwa sababu mimi ndiye mwenyekiti
wa kamati ya maridhiano.”
Pamoja na kupitisha jina la katibu mkuu, vikao vikuu vya Chadema
ambavyo kwa mara ya kwanza vimefanyika nje ya Dar es Salaam, pia
vinatarajiwa kujadili na kuamua mpango mkakati wa kisiasa wa miaka
mitano kuanzia sasa hadi 2021, kupitisha bajeti ya chama kwa kipindi
hicho na kufanya marekebisho ya
katiba, kanuni na miongozo ya mabaraza.
Umeya Dar
Wakati jana Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George
Simbachawene akitangaza kwamba uchaguzi wa Meya wa Dar es Salaam
utafanyika kabla ya Machi 25, Mwalimu na Mnyika walimsihi Rais John
Magufuli kuingilia kati kuepusha balaa inayochochewa na wasaidizi wake
akiwamo waziri huyo.
“Suala la uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ni jipu lililoko
ndani ya Ikulu linalopaswa kutumbuliwa na Rais Magufuli mwenyewe kupitia
nafasi yake ya Waziri wa Tamisemi kwa sababu wizara hii iko chini
yake,” alisema Mnyika.
Wakati Chadema ikitoa malalamiko hayo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa
CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba “Gadafi” amemuomba Waziri
Simbachawene kuangalia utendaji wa kazi wa wakurugenzi wa Manispaa za
Ilala na Kinondoni, akidai wamevuruga uchaguzi wa meya na naibu wake.
Akizungumza na wanahabari jana, Simba alisema CCM imefikia hatua hiyo
baada ya kutoridhishwa na utendaji kazi wa wakurugenzi hao, ikiwamo
kushindwa kutafsiri vyema vifungu vya sheria vilivyosababisha kuondolewa
kwa ya majina ya wajumbe wao kwa madai kuwa hawana sifa za kushiriki
uchaguzi huo.
Chanzo: Mwananchi
Comments