Siri ya mtu atakayerithi nafasi ya katibu mkuu wa Chadema iliyoachwa
wazi na Dk Willibrod Slaa, bado ni ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe.
Kwa mujibu wa ibara ya 7 (13)(b) ya Katiba ya Chadema, mwenyekiti wa
chama ndiye anayetakiwa kupendekeza majina mawili kwenye kikao cha
Baraza Kuu ambacho hupiga kura kumchagua katibu mkuu kati ya wawili yao.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ofisa wa habari wa Chadema,
Tumaini Makene juzi, kikao cha Baraza Kuu kitafanyika Machi 12 jijini
Mwanza, kikitarajia kupokea majina hayo mawili na kuchagua mojawapo kwa
ajili ya kuziba nafasi ya Dk Slaa aliyejiuzulu siasa za vyama tangu
Septemba Mosi, 2015.
Kikao cha baraza hilo kitafuatiwa na Kamati Kuu Machi 13 na Machi 14 kutakuwa na kikao cha Sekretarieti.
“Bado natafakari suala hilo,” alisema Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa tatu wa Chadema tangu ianzishwe mwaka 1992.
Dk Slaa, ambaye aliibukia kuwa katibu mkuu mwenye ushawishi wa chama
hicho kikuu cha upinzani, alijiondoa Chadema kwa madai kuwa ilikubali
kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumpa fursa ya
kugombea urais kabla ya kujisafisha dhidi ya tuhuma za ufisadi
zilizokuwa zikimkabili.
Tangu Dk Slaa ajiondoe, nafasi yake imekuwa ikikaimiwa na Salum
Mwalimu ambaye ni naibu katibu mkuu wa chama hicho upande wa Zanzibar.
Wakati Mbowe akitafakari majina hayo, tayari ubashiri unamtaja Waziri
Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye kuwa mmoja wa watu
wanaopewa nafasi kubwa ya kupendekezwa, sambamba na mnadhimu na
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.
Hata hivyo, Sumaye amekuwa akieleza kuwa hafikirii kushika nafasi
hiyo kwa kuwa umri umeshakwenda na kwamba uamuzi wake wa kujiunga na
chama hicho haukuwa wa kutafuta madaraka.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Lissu hakutaka kuzungumzia
uwezekano wa jina lake kupendekezwa, badala yake alijikita katika
utaratibu wa kikatiba wa kujaza nafasi hiyo.
“Katibu mkuu anatakiwa awe mtu atakayesimamia heshima ndani ya chama,
lazima awe mtu ambaye akisema kitu chama kinasikiliza na nchi
inasikiliza. Pia awe mtu anayekifahamu chama,” alisema Lissu, ambaye pia
ni mwanasheria wa kujitegemea.
“Awe na uwezo wa kuvaa viatu vya Dk Slaa ambavyo si vidogo, ni vikubwa kweli kweli.”
Dk Slaa alijizolea umaarufu kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya
ufisadi pamoja na kulipua mabomu kwenye Serikali ya Awamu ya Nne.
Mbunge huyo wa zamani wa Hanang’ alipitishwa kugombea urais kwa
tiketi ya Chadema mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili, nyuma ya Jakaya
Kikwete.
Alikuwa akitajwa tena kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana,
lakini upepo ulibadilika baada ya Lowassa kujiondoa CCM akipinga
mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho na kujiunga na Chadema.
Chanzo: Mwananchi
Comments