Mshambuliaji Mohamed Mkopi wa timu ya Tanzania Prisons amechaguliwa
kuwa mchezaji bora wa Februari kwa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu wa
2015/2015.
Mkopi katika mwezi huo uliokuwa na raundi nne, alicheza mechi zote
nne za timu yake dhidi ya Mbeya City, Yanga, Mwadui na Mgambo Shooting.
Alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika mechi hizo ambapo zote
ilitoka sare, hivyo kupata jumla ya pointi nne.
Katika mechi hizo ambapo Tanzania Prisons ilifunga mabao matatu,
Mkopi alifunga bao moja na kusaidia kupatikana mabao mengine mawili.
Mshambuliaji huyo ambaye mpaka sasa amefunga mabao sita kwenye Ligi
hiyo, aling’ara zaidi katika mechi mbili kati ya hizo nne ambapo
alichaguliwa kuwa mchezaji bora.
Mkopi ambaye ni mshambuliaji wa kati alichaguliwa mchezaji bora
kwenye mechi dhidi ya Mwadui iliyochezwa mkoani Shinyanga, na ile dhidi
ya Yanga iliyofanyika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya.
Kwa kunyakua tuzo ya mchezaji bora kwa Februari, Mkopi atazawadiwa
kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo,
kampuni ya Vodacom.
Wachezaji bora wa miezi miwili iliyopita ni kiungo Thaban Kamusoko wa
Yanga (Desemba 2015), na beki Shomari Kapombe wa Yanga (Januari 2016).
Comments