Na Salim Said Salim
WASWAHILI wana msemo maarufu unaoeleza kuwa mambo kangaja huenda yakaja.
Sasa wakati waheshimiwa wetu wa Bunge Maalumu la Katiba, baada ya
baadhi yao kutaka waongezwe posho ili watuwakilishe vizuri katika
kuitafutia nchi yetu Katiba mpya wanatarajiwa kuanza kazi iliyowapeleka
Dodoma wakati wowote kuanzia sasa.
Kama wataongezewa posho nawapa hongera kwa kudai ‘haki’ yao na kama watakosa nawapa pole kwa ‘kudhulumiwa’.
Tukumbuke kuwa miaka michache tu iliyopita kuzungumzia kuwepo kwa
Jamhuri ya Tanganyika (aulizwe Mtikila kwa yaliyomkuta na kundi la G55
lilivyofungwa mdomo) na kutaka mfumo wa serikali tatu wa Muungano
ilikuwa ni dhambi kubwa nchini kwetu.
Baadhi ya wale waliothubutu kutoa kauli hizo au kuonyesha ishara ya
kutaka hivyo walipambana na joto ya jiwe na hata baadhi yao kuambiwa
kuwa si raia wa nchi hii. Yale yalikuwa mambo ya unyanyasaji wa hali ya
juu (nawaonea imani waliobuni uchafu ule).
Visa hivi vilipokuwa vinaendelea marehemu rafiki yangu na mwana habari
maarufu aliyeiaga dunia miaka minne iliyopita, Ali Nabwa, alikuwa
akisema wakati ule kuwa kilichohitajika ni subira na ipo siku itakuwa
kweli.
Comments